MKUU wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo, amefanikiwa kumaliza mgomo wa wafanyakazi zaidi ya 1,500 wa Kiwanda cha NAMERA kilichopo Gongolamboto jijini Dar es Salaam, waliokuwa wamegoma wakidai kulipwa mishahara kwa mujibu wa kiwango kipya cha kima cha chini.
Mgomo huo ulitokana na utekelezaji wa Tangazo la Serikali Na. 605A la Oktoba 13, 2025, linaloelekeza ongezeko la wastani wa asilimia 33.4 ya mshahara wa kima cha chini kwa sekta binafsi. Kupitia tangazo hilo, mshahara wa kima cha chini umeongezeka kutoka Sh 275,060 mwaka 2022 hadi Sh 358,222 mwaka 2025.
Akizungumza na wafanyakazi na uongozi wa kiwanda hicho, Mpogolo alisisitiza kuwa utekelezaji wa Amri ya Serikali ni wa lazima kwa waajiri wote, na kwamba hakuna mtu au taasisi inayoruhusiwa kulipa mshahara chini ya kiwango kilichowekwa kisheria, hata kama kuna makubaliano ya ndani kupitia chama cha waajiri au mifumo mingine.
“Amri ya Serikali ni sheria. Haiwezi kupuuzwa wala kubadilishwa kwa makubaliano yoyote. Ni lazima izingatiwe ili kulinda haki za wafanyakazi,” alisema Mpogolo.
Aidha, alitoa maelekezo kwa uongozi wa kiwanda kuhakikisha mishahara inalipwa kwa mujibu wa Tangazo la Serikali Na. 605A la mwaka 2025, huku akibainisha kuwa hakuna mfanyakazi atakayefukuzwa kazi kwa sababu ya kushiriki mgomo huo. Alisema hatua hiyo inalenga kujenga mahusiano bora kati ya waajiri na waajiriwa na kuimarisha utulivu kazini.
Mpogolo pia alikitaka kiwanda kushirikiana kwa karibu na Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara na Taasisi za Fedha (TUICO) pamoja na Afisa Kazi wa Mkoa wa Dar es Salaam ili kufanikisha uchaguzi wa viongozi wa wafanyakazi watakaokuwa kiungo kati ya wafanyakazi na uongozi. Vilevile alisisitiza umuhimu wa kupitia mikataba ya ajira ili ihakikishe inazingatia sheria na kanuni za kazi.
Akizungumza kuhusu mchango wa kiwanda hicho kwa jamii, Mpogolo alisema ni muhimu kulinda uwepo wake kutokana na nafasi zake kubwa za ajira na mchango wake katika uchumi wa taifa. “Migogoro ya mara kwa mara inaweza kuhatarisha ajira na ukuaji wa uchumi. Ndiyo maana leo nimehakikisha mgogoro huu unamalizika kwa amani,” aliongeza.
Kwa upande wao, wafanyakazi wa kiwanda hicho wameeleza kuridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Mkuu wa Wilaya huyo, wakisema zimewarejeshea matumaini na kuimarisha mazingira ya kazi. Wameahidi kurejea kazini mara moja na kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa bidii kama ilivyokuwa awali.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Ilala, ACP Yustino Mgonja, amepongeza juhudi za Mpogolo katika kushughulikia mgogoro huo kwa haraka na busara, akibainisha kuwa hali ya usalama katika eneo la kiwanda ni shwari na kwamba wafanyakazi na mali zao viko salama.





Toa Maoni Yako:
0 comments: