Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini, IGP Camillus Wambura, amefungua rasmi mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kiutendaji Sekretarieti ya Maadili ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dodoma, yanayofanyika katika Chuo cha Taaluma ya Polisi Dar es Salaam (DPA) kuanzia tarehe 15 hadi 19 Disemba, 2025.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, IGP Wambura, alisisitiza kuwa. mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha watendaji kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uwajibikaji na uadilifu mkubwa zaidi ili kuendelea kutoa huduma bora kwa jamii.
Alibainisha kuwa, mafunzo hayo yataimarisha uwezo wa washiriki katika kusimamia maadili, kushughulikia malalamiko ya wananchi, kuandaa taarifa za robo mwaka na mwaka pamoja na kutumia kikamilifu Mfumo wa Kielektroniki wa Kushughulikia Mrejesho (e-Mrejesho) ili kuongeza uwazi na ufanisi ndani ya Jeshi la Polisi.
Aidha, IGP Wambura alisisitiza umuhimu wa maadili kwa viongozi, akieleza kuwa mmomonyoko wa maadili kwa viongozi wa juu huathiri mwenendo wa taasisi nzima na kuwataka washiriki kuwa mfano bora wa maadili mema ili kulinda taswira ya Jeshi la Polisi na kuendeleza imani ya wananchi kwa jeshi hilo.
Akihitimisha hotuba yake, IGP Wambura aliwataka washiriki kuzingatia sheria, kanuni na miongozo iliyopo katika kushughulikia malalamiko, kupambana na vitendo vya rushwa na ukiukwaji wa maadili bila upendeleo, huku akieleza kuwa mafunzo hayo ni chachu ya kuimarisha Nidhamu, Haki, Weledi na Uadilifu ndani ya Jeshi la Polisi Tanzania.
Kwa upande wake, Kamishna wa Utawala na Menejimenti ya Rasilimali Watu wa Jeshi la Polisi, CP Tatu Jumbe, akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa yatalenga kuwajengea uwezo washiriki kutambua na kutekeleza kikamilifu majukumu ya Kamati ya Kusimamia Maadili na Ushughulikiaji wa Malalamiko pamoja na Watendaji wa Sehemu (Chiefdom) ya Maadili na Malalamiko.





Toa Maoni Yako:
0 comments: