Na WMJJWM – Tunisia

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameshiriki Mkutano wa 6 wa Ngazi ya Juu kuhusu Masuala ya Wanawake, Amani na Usalama (WPS) uliofanyika tarehe 9–10 Desemba 2025 katika Chuo cha Kimataifa cha Diplomasia, jijini Tunis nchini Tunisia.

Akizungumza katika mkutano huo, Dkt. Gwajima ameupongeza Umoja wa Afrika kupitia Ofisi ya Mjumbe Maalum wa AU wa Masuala ya Wanawake, Amani na Usalama, pamoja na Serikali ya Tunisia kwa kuandaa mkutano huo muhimu wenye mstakabali wa Wanawake.

Akiwasilisha mchango wake katika mjadala wa jopo la wataalamu, Dkt. Gwajima amesema kasi ya ukuaji wa teknolojia na akili mnemba imekuwa na manufaa pale inapowezesha jamii kuelimishwa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia, sambamba na kusambaza ujumbe wa kukataa vitendo hivyo.

Dkt. Gwajima pia ameeleza mafanikio makubwa yaliyofikiwa na Tanzania, ikiwemo kuzinduliwa kwa Mpango wa Taifa wa Kwanza wa Wanawake, Amani na Usalama (TNAP), mageuzi ya sera na sheria kama Sheria ya Uchaguzi ya 2024, pamoja na ongezeko la uwakilishi wa wanawake katika nafasi za maamuzi serikalini. Aidha, amebainisha hatua za serikali kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia mikopo ya asilimia 10 ya halmashauri na juhudi za kitaifa za kupambana na ukatili wa kijinsia.
Amesema mkutano huo unatoa fursa ya kutathmini mafanikio ya utekelezaji wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, pamoja na kubainisha changamoto na mikakati mipya ya kuimarisha utekelezaji wake barani Afrika.

Dkt. Gwajima ameeleza kuwa licha ya hatua nzuri zilizopigwa katika kupanua usawa wa kijinsia, wanawake bado wanakabiliwa na vikwazo mbalimbali huku akitaja mila na desturi kandamizi, changamoto za kiuchumi na athari wanazokutana nazo wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi za uongozi kuwa miongoni mwa mambo yanayopunguza ushiriki wao katika uongozi na siasa.

Amesisitiza kuwa utekelezaji wenye tija wa ajenda ya WPS unahitaji ushirikiano mpana kati ya serikali, mashirika ya kiraia, wadau wa maendeleo na taasisi za kikanda huu akisema Tanzania itaendelea kushirikiana na Umoja wa Afrika na wadau wengine ili kuhakikisha wanawake wanapata nafasi stahiki katika meza za maamuzi na michakato ya ujenzi wa amani barani Afrika.

Hata hivyo, ameonya kuwa teknolojia hiyo hiyo imekuwa ikichochea aina mpya za ukatili wa kijinsia mtandaoni, ambao waathirika wakubwa ni wanawake na wasichana.

Amefafanua kuwa mitandao ya kijamii imekuwa ikitumika kusambaza video za uongo, chuki, vitisho na matusi yanayolenga kuwachafua wanawake hadharani, jambo linalotishia usalama wao mtandaoni na kuwavunja moyo wanaotaka kushiriki katika uongozi na siasa.

Aidha amehimiza wadau wote kushiriki kikamilifu katika kutoa hamasa na elimu juu ya matumizi salama ya mitandao ili kulinda wanawake, wasichana na jamii kwa ujumla.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: