Luangwa, Zambia – Jumamosi, 27 Septemba 2025: Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, ameihakikishia jamii ya Luangwa na wananchi kwa ujumla kuwa serikali imejipanga kuchukua hatua thabiti za kupunguza migongano kati ya binadamu na wanyamapori ili kulinda maisha na mali za wananchi.
Akihutubia kupitia Waziri wa Uvuvi na Mifugo, Peter Kapala, wakati wa sherehe za jadi za Dantho za watu wa Chikunda wilayani Luangwa, Rais Hichilema alisema serikali inaendelea kulinda rasilimali za asili huku ikihakikisha jamii zinanufaika na utalii endelevu.
Rais Hichilema alikiri kuwa migongano ya binadamu na wanyamapori imeathiri maisha ya wananchi wilayani humo, ikiwemo mazao kuharibiwa na vifo vya watu, hali inayotishia usalama wa chakula.
Kama hatua ya awali ya kupunguza tatizo hilo, serikali imenunua magari mawili aina ya Land Cruiser kwa Idara ya Hifadhi za Taifa na Wanyamapori ili iweze kuitikia kwa haraka matukio ya wanyama kushambulia wananchi na mashamba yao.
"Nataka nieleze kuwa hatua hizi tulizoweka zinakusudia kujenga usawa na maelewano kati ya binadamu na wanyamapori," alisisitiza Rais Hichilema.
Aidha, aliushukuru Uongozi wa Kiasili wa Chikunda, hususan Chifu Mphuka, kwa kuendeleza shughuli za kilimo wilayani Luangwa. Alibainisha kuwa serikali imepanua msaada kwa wakulima kupitia mpango wa Farmer Input Support Program (FISP) na Sustainable Agricultural Financing Facility.
Kupitia programu hizo, wakulima wamepata fursa ya mikopo ya kununua vifaa vya umwagiliaji, pembejeo za kilimo, zana za kisasa na mifugo.
"Hatua hizi ni za kipekee katika kuwawezesha wakulima wetu na kusukuma mbele kibiashara sekta ya kilimo nchini Zambia," alisema Rais Hichilema huku akiahidi serikali itaendelea kuwafikia wakulima wengi zaidi.
Rais pia alisisitiza mshikamano kati ya serikali na viongozi wa jadi, akiahidi kuendelea kuunga mkono sherehe za kitamaduni zinazochangia kudumisha amani, mshikamano wa kitaifa na maendeleo ya kijamii.
Kwa upande wake, Chifu Mphuka aliishukuru serikali kwa kupeleka miradi ya maendeleo na mipango ya ulinzi wa kijamii katika eneo lake, akitaja social cash transfer na cash for work kuwa zimewanufaisha kaya nyingi.
Sherehe za mwaka huu za Dantho zimebeba kaulimbiu isemayo: “Urejeshaji wa Utamaduni kwa Umoja wa Kitaifa, Amani na Maendeleo ya Uchumi wa Zambia baada ya Miaka 60.”



Toa Maoni Yako:
0 comments: