Na Mwandishi Wetu – Dodoma
Balozi wa Italia nchini Tanzania, Mheshimiwa Giuseppe Sean Coppola, tarehe 4 Agosti 2025, alitembelea Kituo cha Taifa cha Ufuatiliaji wa Majanga na Tahadhari ya Mapema kilichopo Mtumba, jijini Dodoma, kwa lengo la kujionea utendaji wa kituo hicho na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Italia katika sekta ya usimamizi wa maafa.
Katika ziara hiyo, Balozi Coppola alipokelewa na Mkurugenzi Msaidizi wa Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura, Bi. Jane Kikunya. Alifuatana na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Italia (AICS) kwa Kanda ya Afrika, Bw. Fabio Minniti, pamoja na wataalamu wa shirika hilo, Bw. Paolo Razzini na Bi. Sara Pini.

Ujumbe huo ulipata fursa ya kujionea kwa karibu namna kituo hicho kinavyofanya kazi ya kufuatilia matukio ya majanga, kutoa tahadhari ya mapema, na kusaidia mipango ya haraka ya kukabiliana na athari zake. Kituo hicho ni sehemu ya miradi iliyofadhiliwa na Serikali ya Italia kwa kushirikiana na Serikali ya Tanzania, ikiwa na lengo la kuimarisha mfumo wa kitaifa wa tahadhari na usimamizi wa maafa.
Akizungumza baada ya ziara hiyo, Balozi Coppola alieleza kufurahishwa na hatua zilizopigwa na kituo hicho katika kuhakikisha usalama wa wananchi dhidi ya majanga. Aliahidi kuwa Serikali ya Italia itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kuimarisha mifumo ya kiteknolojia, mawasiliano ya haraka, na utoaji wa tahadhari kwa wakati.
"Serikali ya Italia imejizatiti kushirikiana na Tanzania katika kujenga uwezo wa kitaasisi na kiteknolojia kwa ajili ya kudhibiti majanga, kupunguza madhara, na kulinda maisha ya watu wake," alisema Balozi Coppola.

Kwa upande wao, wataalamu wa AICS walisisitiza dhamira yao ya kuendeleza ushirikiano na wataalamu wa ndani kupitia mafunzo ya kitaalamu,. uboreshaji wa miundombinu ya TEHAMA, na utekelezaji wa miradi endelevu ya kujenga jamii thabiti dhidi ya majanga ya asili pamoja na yale yanayosababishwa na shughuli za kibinadamu.
Ziara hiyo imetajwa kuwa sehemu ya juhudi za kudumisha ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na Italia katika maeneo ya maendeleo endelevu, ulinzi wa maisha ya wananchi, pamoja na usimamizi wa rasilimali na mazingira.










Toa Maoni Yako:
0 comments: