Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Dotto Biteko (wa tatu kutoka kulia), akiwa katika uzinduzi Rasmi wa tawi la benki ya Exim Tanzania wilayani Kahama mkoani Shinyanga. Kulia kwake ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank, Bw. Jaffari Matundu wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali na benki ya Exim katika tukio lililofanyika mnamo tarehe 25 Februari 2025 mjini Kahama.
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Dkt. Doto Biteko (wa tatu kutoka kushoto), ambaye alikuwa Mgeni Rasmi akikata utepe wakati hafla ya uzinduzi Rasmi wa tawi la benki ya Exim wilayani Kahama mkoani Shinyanga Wa pili kutoka kushoto ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Exim Bank, Bw. Jaffari Matundu na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha (wa nne kutoka kushoto) wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wa Serikali na benki ya Exim katika tukio hilolilofanyika mnamo tarehe 25 Februari 2025 mjini Kahama.
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga.
25 Februari 2025, Shinyanga: Benki ya Exim imedhihirisha dhamira yake ya kujenga ujumuishi wa kifedha na kupanua huduma zake kwa kuzindua rasmi tawi jipya katika Wilaya ya Kahama, Mkoani Shinyanga. Tawi hili jipya linalenga kuboresha upatikanaji wa huduma za kifedha kwa wafanyabiashara, watu binafsi, na taasisi katika wilaya hiyo. Mgeni rasmi katika hafla hii alikuwa Mheshimiwa Doto Biteko, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Exim, Bw. Jaffari Matundu, alieleza umuhimu wa upanuzi huu kwa ukuaji wa sekta ya kifedha: "Kahama ni moja ya vituo muhimu vya uchumi nchini, ikiwa na sekta zinazochangia kwa kiasi kikubwa kwenye maendeleo ya taifa. Mji huu unajulikana sana kwa mchango wake katika sekta ya madini, hususan uzalishaji wa dhahabu, ambao umeifanya Kahama kuwa muhimu katika uchumi wa taifa.”
Jaffari aliongeza kuwa, “Kwa kuanzisha tawi hili, tunalenga kuhudumia mahitaji mbalimbali ya kifedha ya sekta hizi—iwe ni kwa ufadhili wa biashara, huduma za kibenki za kidijitali, au bidhaa za kifedha zinazolenga kukuza maendeleo ya kiuchumi.”
Tawi la Kahama litatoa huduma kamili za kibenki, ikiwemo akaunti za biashara na binafsi, huduma za hazina (treasury services), na mifumo ya kidijitali ya kibenki. Wateja watanufaika na huduma za Exim Bank zinazolenga kutoa suluhisho bora, la kisasa, na lenye ushindani kwa kuzingatia mahitaji ya soko yanayobadilika kila wakati.
Mheshimiwa Doto Biteko, alisifu juhudi za benki ya Exim za kupanua huduma zake, akisisitiza mchango wa taasisi za kifedha katika maendeleo ya Uchumi wa watu na taifa kiujumla:
“Serikali imekuwa ikihimiza taasisi zetu kuipeperusha bendera ya Tanzania nje ya nchi kwa kufanya uwekezaji wa kimkakati. Kwa kipekee kabisa niwapongeze sana Exim bank kwa kutuwakilisha vyema katika nchi za Comoros, Uganda, Djibouti, pamoja na Ethiopia.”
“Serikali imeweka mkazo mkubwa katika kuhakikisha huduma za kifedha zinawafikia Watanzania wengi zaidi, hasa wale walioko nje ya mifumo rasmi ya kifedha. Kwa niaba ya Serikali, naomba nitumie fursa hii kuipongeza Exim Bank kwa hatua hii kubwa na kwa jitihada zenu za kuleta huduma za kifedha karibu zaidi na wananchi,” alisema Mhe. Biteko.
Tawi hili jipya linaonesha azma ya benki ya Exim ya kutoa suluhisho rahisi na jumuishi za kifedha huku ikiongeza uwepo wake katika maeneo muhimu kote Tanzania. Kwa kujikita katika ubunifu na utoaji wa huduma bora kwa wateja, benki ya Exim inaendelea kuwa mshirika muhimu wa maendeleo ya kifedha nchini.
Kadri benki ya Exim inavyoendelea kupanua huduma zake Kahama, benki hii inaendelea kushikilia dhamira yake ya kuwawezesha watu binafsi na wafanyabiashara kwa huduma za kifedha zinazopatikana kwa urahisi, za kuaminika, na za kisasa.
Upanuzi huu ni sehemu ya mkakati mpana wa benki wa kuchochea maendeleo ya uchumi, kuimarisha biashara za ndani, na kuongeza uelewa wa masuala ya kifedha katika jamii. Kwa mtazamo unaoweka mteja mbele na dira ya mafanikio ya muda mrefu, benki ya Exim iko tayari kubadilisha huduma za kifedha na kuleta maendeleo endelevu nchini Tanzania.
Toa Maoni Yako:
0 comments: