Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mjumbe wa Tume, Dkt. Zakia Mohamed Abubakar.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga akifunga mafunzo hayo kwa niaba ya Mjumbe wa Tume, Dkt. Zakia Mohamed Abubakar.
Mwenyekiti wa Mafunzo, Bw. Khalid Khalif akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo.
Na Mwandishi wetu, Songea
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga kura mkoani Ruvuma wametakiwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao baadae mwaka huu.
Hayo yamesemwa na Mjumbe wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Dkt. Zakia Mohamed Abubakar kupitia hotuba yake iliyosomwa kwa niaba yake na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura (Elimu) Dkt. Rose Likangaga wakati akifunga mafunzo ya siku mbili kwa watendaji hao mkoani Ruvuma.
“Mnahimizwa kuhamasisha wananchi wenye sifa ili wajitokeze kujiandikisha na kupata haki yao ya kikatiba itakayowawezesha kushiriki katika kuchagua viongozi wao,” ilisema sehemu ya hotuba hiyo.
Dkt Likangaga akisoma hotuba hiyo alisema ni matarajio ya Tume kuwa, mara baada ya zoezi hili lililopo mbele yao kukamilika watu watakaokuwa wamepatiwa kadi watakuwa ni Wapiga Kura Halali.
Aidha alisema, jukumu la uhamasishaji linawahusu moja kwa moja wao watendaji kwa kushirikiana na wadau wengine katika maeneo yao kupitia nyenzo walizonazo.
“Ninasisitiza kwamba, mabango na vipeperushi mtakavyopewa na Tume mvisambaze mapema katika kata zote zilizopo katika halmashauri zenu. Kazi yenu kubwa ni kusimamia na kuendesha shughuli zote za uboreshaji katika halmashauri zenu,”ilisisitiza hotuba hiyo.
Watendaji hao wameatakiwa kuisoma kwa umakini Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sheria za Uchaguzi, Kanuni za Uboreshaji, Maelekezo na Miongozo yote inayotolewa na Tume ili kazi yao ifanyike kwa uadilifu na haki.
Pia wametakiwa kuwasiliana na Tume kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala yote yanayohusiana na utekelezaji wa majukumu yao pindi wanapokutana na changamoto zozote.
“Tume imetekeleza jukumu lake katika hatua ya mafunzo na hivyo nanyi mna wajibu wa kuhakikisha kuwa mnatekeleza kikamilifu majukumu yote mliyokasimiwa,” ilisema sehemu ya hotuba hiyo.
Pia Tume imewataka watendaji hao kuwa makini katika kila eneo la usambazaji na utunzaji wa vifaa na muda sahihi wa ufunguaji na ufungaji wa vituo vya kuandikishia wapiga kura.
Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unataraji kuanza Januari 12 hadi 18, 2025 katika mikoa ya Songwe, Njombe, Rukwa na Ruvuma kwenye Halmashauri za Wilaya ya Nyasa, Mbinga, Mbinga Mji, Wilaya ya Songea na Manispaa ya Songea ambapo vituo vitakuwa vinafunguliwa kuanzia saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
Mafunzo hayo yaliwahusisha Maafisa Waandikishaji,Maafisa Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi, Maafisa TEHAMA wa Halmashauri.
Washiriki wakisikiliza hotuba ya kufunga mafunzo hayo.
Mafunzo yakiendelea
mmoja wa wakufunzi akitoa maelekezo wakati wa mafunzo kwa vitendo.
Washiriki wakifanya mafunzo kwa vitendo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: