Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Kigoma.
Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhe. Nape Moses Nnauye (Mb) amezitaka Kampuni za Simu zilizopewa miradi ya ujenzi wa Minara 8 ya Mawasiliano ya Simu katika Mkoa wa Kigoma kuhakikisha inakamilika hadi kufikia Oktoba mwaka huu.

Waziri Nape amesema kukamilika mapema kwa ujenzi wa minara hiyo kutawezesha wananchi zaidi ya 108,126 wanaopata changamoto ya Mawasiliano kwa sasa katika Kata Nane za Mkoa wa Kigoma kupata huduma hiyo.
Amesema hayo tarehe 15 Julai, 2024 wakati akizungumza na Viongozi mbalimbali wa Mkoa wa Kigoma, Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo na watoa huduma za Mawasiliano, mara baada ya kupokea taarifa ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) na Mamlaka ya Mawasiliano Tannzania (TCRA) kuhusu hali ya upatikanaji wa Huduma za Mawasiliano na mradi wa ujenzi wa Minara katika mkoa huo.
"Vodacom mna minara 4 ambayo bado hamjaanza kujenga, tukubaliane hadi kufikia Oktoba, 2024 iwe imekamilika, nimeshaongea na Mtendaji Mkuu sitaki ifike Oktoba, 2024 tuanze kukabana koo, fedha mmeshapokea malizeni ujenzi wa mnara, TTCL nao nataka Oktoba, 2024 pia kazi iwe imeisha wana Kigoma waanze kunufaika na Uchumi wa Kidigitali," amesema Waziri Nape.

Amesema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), inahakikisha inawaunganisha Watanzania kwa mawasiliano yenye sifa tano ambazo ni upatikanaji, ubora, usalama, yenye matokeo chanya na anayoweza kumudu mtu yeyote hata wa kipato cha chini.

"Zimekuja bilioni 1.38 katika Mkoa wako (Mkuu wa Mkoa Mhe. Thobias Andengenye) kwa ajili ya ujenzi wa minara na tutafanya scanning, niwaagize UCSAF na TCRA kwa kuwa huu ni mkoa wa pembezoni vizuri tukaongeza fedha ili yale maeneo ambayo yako wazi katika miradi inayokuja tuongeze nguvu ili kuhakikisha tunawaunganisha Watanzania wote na hakuna anayeachwa nyuma," amesema.

Amemuomba Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Mhe. Thobias Andengenye, Wakurugenzi na Wakuu wa Wilaya kuwa wepesi wa kusaidia upatikanaji wa ardhi na kuidhinisha vibali kwa ajili ya ujenzi wa minara kwa wakati ili wananchi waweze kupata huduma za mawasiliano.

"..Wakati mwingine inachukua miezi sita kupata vibali, 'this is too much', ukiangalia hapa kuna minara haijajengwa na nilikuwa nazungumza na watoa huduma wanasema hizi taratibu za utoaji vibali na ardhi za kijiji zinaleta shida, hii siyo sawa," amesema.

Aidha Waziri Nape amemuomba Mkuu huyo wa Mkoa kuzungumza na TARURA na REA ili zitoe kipaumbele cha kupeleka huduma za miundombinu ya Barabara na Umeme kwenye maeneo yote inakojengwa Minara ili kusaidia kupunguza gharama za uendeshaji wake na hivyo wananchi wapate mawasiliano saa 24.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: