Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Abdallah Ulega amefika Wilayani Hanang, Mkoani Manyara kwa lengo la kutoa pole na kukabidhi mchango wa wadau na wizara kwa wananchi walioathirika na mafuriko wilayani humo.

Wakati akitoa salamu hizo za pole Disemba 11, 2023, Mhe. Ulega alisema kuwa Wizara yake imepokea kwa masikitiko makubwa tukio la mafuriko hayo yaliyotokea na kusababisha kupotea kwa maisha ya watanzania pamoja na uharibifu wa mali na mifugo.

Aliendelea kufafanua kuwa kufuatia kadhia hiyo, Wizara yake kwa kushirikiana na wadau katika sekta ya mifugo na uvuvi wakiwemo ASAS, Bajuta International, Dalberg International, Karie Kinana, APOKA, TAFMA, TABROFA na TPBA) kwa pamoja wameandaa vitu mbalimbali na kuvikabidhi kwa Kamati ya Maafa ya Kitaifa kwa ajili ya uratibu wa namna nzuri ya kuvifikisha kwa familia na walengwa wote.

Miongoni mwa vitu hivyo ambavyo amevikabidhi ni pamoja na Ng’ombe 13, Mbuzi 20, Trei 90 za mayai, Fedha tasilimu jumla ya shilingi Milioni 5, Maziwa katoni 300, Sembe, Maharage na Chumvi.

"Kufuatia tukio hili lililoumiza mioyo ya watanzania wote, Wizara yangu inaungana na Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan kutoa pole kwa familia zote zilizopatwa na matatizo", alisema

Aidha, alibainisha kuwa Wizara yake itaendelea kushirikiana na Kamati ya Taifa ya Maafa na Uongozi wa Mkoa na Wilaya ili kubaini uharibifu wote wa miundombinu ya mifugo na kuirejesha katika hali yake kwa haraka ili kuhakikisha mifugo inaendelea kupata huduma stahiki na kuwezesha wafugaji kunufaika na mifugo yao kwa maendeleo ya nchi.

Waziri Ulega aliendelea kusisitiza kuwa Serikali inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimama na watanzania wote katika hali zote ambazo zinawapata watanzania akiongeza kuwa wao kama wasaidizi wake wapo imara kuhakikisha adhma yake ya kuendelea kuwaletea maendeleo Watanzania inatimia.

Waziri Ulega amekabidhi vifaa hivyo kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Mhe. Jenista Mhagama kwa niaba ya waathirika wa mafuriko hayo.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mhe. Queen Sendiga alitoa shukrani zake za dhati kwa Mheshimiwa Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan na Wadau mbalimbali wanaoendelea kujitokeza kuwafariji katika kipindi hiki kigumu.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: