Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akizungumza na wawakilishi kutoka Vyama vya Siasa kuhusu majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanayotarajiwa kufanyika katika Kata za Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
Sehemu ya viongozi wa vyama vya siasa vikishiriki katika mkutano huo wa Tume na Vyama vya siasa.
Sehemu ya viongozi wa vyama vya siasa vikishiriki katika mkutano huo wa Tume na Vyama vya siasa.
Viongozi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) nao wakiwa katika mkutano hao.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uboreshaji wa majaribio wa Daftari La Kudumu la Wapiga Kura.
BVR Kits zenye vifaa mbalimbali vinavyowasiliana ili kuchukua na kutunza taarifa za wapiga kura BVR Kits za sasa ambazo zinatumia programu ya android tofauti na BVR Kits za awali ambazo zilikuwa zinatumia programu ya Microsoft Windows.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele akifafanua jambo wakati wa majadiliano.
Viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa wakichangia mada wakati wqa mkutano huo wa Tume na Vyama vya siasa katika Ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam leo Novemba 16,2023.
Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Bw. Ramadhani Kailima akifafanua jambo wakati wa mjadala na wawakilishi wa vyama vya siasa.
Na Mwandishi Wetu.
Vyama vya siasa vimehimizwa kushiriki kwenye majaribio ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura yanayotarajiwa kufanyika katika Kata za Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora, Mkoa wa Tabora na Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Mkoa wa Mara kuanzia tarehe 24 hadi 30 Novemba, 2023.
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji (Rufaa) Jacobs Mwambegele ametoa wito huo leo tarehe 16 Novemba, 2023 wakati akifungua mkutano wa Tume na vyama vya siasa jijini Dar es Salaam.
“Vyama vya siasa kwenye zoezi hili vitashiriki kwa kuweka wakala mmoja katika kila kituo cha kuandikisha wapiga kura, lengo ni kushuhudia na kujiridhisha juu ya taratibu zitakazotumika wakati wa majaribio ya uboreshaji wa Daftari,” amesema Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa majaribio ya uboreshaji yanafanyika kwa lengo la kupima uwezo wa vifaa na mifumo itakayotumika wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura unaotarajiwa kufanyika nchi nzima kwa tarehe zitakazopangwa na kutangazwa na Tume.
Majaribio ya uboreshaji yatahusisha kuandikisha raia wa Tanzania mwenye umri wa miaka 18 au zaidi na atakayetimiza umri wa miaka 18 kabla au ifikapo tarehe ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Kundi lingine litakalohusika kwenye zoezi hili ni; wapiga kura wanaoboresha taarifa zao ambao wamehama kutoka eneo moja la uchaguzi kwenda eneo lingine, waliopoteza au kadi zilizoharibika, wanaorekebisha taarifa zao na kuondoa wapiga kura waliopoteza sifa za kuwemo katika Daftari.
Majaribio ya uboreshaji yatafanyika katika vituo 16 vya kuandikisha wapiga kura. Kati ya hivyo, vituo 10 ni vya Kata ya Ng’ambo na vituo sita (6) ni kutoka Kata ya Ikoma. Vituo vya uandikishaji vitafunguliwa saa 2:00 asubuhi na kufungwa saa 12:00 jioni.
“Tume ya Uchaguzi inatoa wito kwa wakazi wa Kata ya Ng’ambo iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora na Kata ya Ikoma iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, kujitokeza kwa wingi kushiriki katika majaribio ya uboreshaji wa Daftari na kutoa ushirikiano kwa Tume wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hili muhimu kwa mustakabali wa Taifa,” amesema Jaji Mwambegele.
Toa Maoni Yako:
0 comments: