Na Janeth Raphael

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, leo Juni 13 amewataka wafanyabiashara wa mazao kutafuta vibali stahiki vya kusafirisha mazao kabla ya kuanza kuyanunua kwa wakulima

Alivitaja vibali hivyo kuwa ni kama vile kibali cha kusafirisha mazao nje ya nchi na cha usafi wa mazao (Phytosanitary)

Bashe ametoa agizo hilo kwa wafanyabiashara leo katika kikao chake na Vyombo vya Habari kilicholenga kutoa suluhisho kwa malori yaliyokwama mipakani hususan mpaka wa Tanzania na Kenya- Namanga ambapo kuna malori zaidi ya 40 yamekwama yakiwa yamebeba mazao mbalimbali.

Bashe alisema, imekuwa ni tabia kwa wafanyabiashara hao kuanza kukusanya mazao ya wakulima bila ya kuwa na vibali vya kuyasafirisha na kisha kuanza kutafuta vibali wakifika mpakani.

Alisema, tukio hilo ni mara ya pili kutokea ambapo kwa awali lilipotokea serikali iliwasamehe na kuruhusu kusafirisha mazao na tukio la sasa pia inawasamehe wasafirishe mazao lakini amewakanya kuwa haitokuwa na msamaha tena.

“Hili tukio la sasa hivi ni mara ya pili linajitokeza ambapo awali walisamehewa na kwa kuwa serikali haitaki kuwaumiza wakulima kwa kuzuia kusafirishwa kwa mazao hayo na hili la sasa tunawasamehe, ila iwe ndiyo mwanzo na mwisho wakirudia tena mazao yao yote tutachukua.” alisema Bashe.

Alisema vibali vinatolewa bure kwa njia ya mfumo ATMIS mtandaoni hivyo hakuna sababu ya wafanyabiashara hao kukwepa kutafuta huku akiwataka pia kuwa na vibari vya tathmini ya mazao.

Alisema faida ya kuwa na vibali hivyo ni kuwezesha kupatikana kwa takwimu sahihi kuhusu kiwango cha mazao kinachosafirishwa nje ya nchi na nchi yanapokwenda ili kuondoa mwanya wa watu wengine kupeleka mazao yasiyokuwa na kiwango kwenye nchi hizo kisha kusingizia kuwa yametoka Tanzania.

Kutokana hali hiyo Bashe alisema kuwa serikali haitosita kuyachukua mazao yatakayokamatwa tena siku nyingine yakisafirishwa bila vibali
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: