Serikali imesema Tanzania inawanasayansi mahili na wabunifu wenye vipawa na uwezo wa kutoa changamoto katika kujenga uchumi na kuboresha maisha ya mtu mmoja mmoja.
Kauli hiyo imetolewa Naibu Waziri Wa Elimu, Sayansi Na Teknolojia Mhe. Omary Juma Kapinga wakati akifungua Maonesho ya Saba ya wiki ya Utafiti na Ubunifu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) yanayofanyika Jijini Dar es Salaam.
"Ndugu zangu, serikali inatambua mchango wa utafiti na ubunifu kama nyenzo muhimu katika kuboresha na kurahisisha maisha kwa kuokoa muda katika utendaji wa kazi kuongeza tija na ubora katika uzalishaji wa bidhaa na utoaji wa huduma," amesema Mhe. Kapinga.
Aidha, amesema utafiti na ubunifu ni maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi ambavyo vinakwenda sambamba hivyo ni lazima lazima watafiti, wabunifu na wavumbuzi katika sekta zote wachukue hatua za makusudi kubuni na kuzalisha teknolojia kwa ajili ya kuleta maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika jamii.
Mwisho ameupongeza uongozi wa UDSM kwa kuendelea kulea watafiti, wabunifu na wavumbuzi katika sekta zote.
Maonesho ya Saba ya Wiki Ya Utafiti na Ubunifu Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam yanameanza rasmi Mei 24 hadi 26, 2022, Katika Maktaba Mpya Ya Chuo Kikuu Cha Dar es Salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments: