Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim majaliwa (kushoto) na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo (kulia) wakifungua kitambaa kuashiria uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa Ufundi tower katika Chuo cha Ufundi Arusha, Jijini Arusha.
Naibu Katibu wa Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Carolyne Nombo akiongea na hadhara iliyohudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika jengo la Ufundi tower lililopo Chuo cha Ufundi Arusha, Jijini Arusha.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim majaliwa akiongea na hadhara iliyohudhuria hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika jengo la Ufundi tower lililopo Chuo cha Ufundi Arusha, Jijini Arusha.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim majaliwa akiangalia mchoro wa jengo la Ufundi tower lililopo Chuo cha Ufundi Arusha wakati akikagua mradi wa ujenzi wa jengo hilo Jijini Arusha.

SERIKALI itaendelea kutoa fedha za kuboresha miundombinu ya Vyuo vya Ufundi ili wanafunzi wa Kitanzania waendelee kupata elimu katika mazingira bora.

Hayo yamesemwa leo Mei 24, 2022 Jijini Arusha na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) wakati akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la maabara, madarasa na ofisi (Ufundi Tower) katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).

Amesema Serikali imetoa fedha nyingi kwa ajili ya kuboresha sekta ya Elimu kuanzia Awali hadi Vyuo Vikuu kwa wanafunzi wa kawaida na wenye mahitaji maalum.

"Tumejenga madarasa, mabweni, maabara za masomo ya sayansi, tumeongeza nyumba za walimu, majiko na mabwalo ili watoto wa Kitanzania waweze kupata elimu bora bila changamoto yoyote," amesema mhe. Majaliwa.

Mhe. Majaliwa ameongeza kuwa Serikali pia inafanyia kazi suala la upatikanaji wa mikopo kwa wanafunzi wa ngazi ya Diploma kupitia tume ya kutathmini iliyoundwa na Wizara ya Elimu ili kuona namna ya kuweza kutoa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ngazi ya kati.

"Kupitia bajeti ya mwaka huu ambayo inafikia bilioni 570 tunataka tuone kila mwanafunzi wa Kitanzania anayetoka kwenye familia isiyokuwa na uwezo wa kujilipia gharama mbalimbali ananufaika na mkopo huo," amefafanua Mhe. Majaliwa.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Carolyne Nombo akiongea katika hafla hiyo kwa niaba ya Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe Prof. Adolf Mkenda (Mb) amesema Wizara ilipokea jumla ya Shilingi bilioni 64.9 kutoka kwenye fedha za Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko 19 ambazo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kielimu.

"Mradi huu ulioweka jiwe la msingi leo ni matokeo ya jitihada kubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita lakini pia na ushawishi mkubwa wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kuweza kupata fedha hizo ili kuweza kukamilisha miradi hii," amesema Prof. Nombo.

Ameongeza kuwa pamoja na kuwa Uviko imekuwa ni changamoto lakini kwa Tanzania imekuwa ni baraka pia kwa kuwa fedha zake zimeweza kutumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha miundombinu ya kufundishia na kujifunzia.

"Fedha hizi zimeelekezwa katika Vyuo vya VETA 25 vya Wilaya, vinne vya mikoa, Vyuo vya Ualimu ambako tumejenga madarasa, mabweni na kumbi la mihadhara kwa lengo la kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia," amefafanua Prof. Nombo.

Naye Mkuu wa Chuo cha Ufundi Arusha, Dkt. Musa Chacha amesema ujenzi wa jengo la ufundi tower ulianza Januari 2022 na unatarajiwa kukamilika mwisho wa mwezi Juni 2022.

"Jengo hili lina ghorofa tatu na litakuwa na maabara, madarasa, ofisi na stoo na ujenzi wake mpaka sasa umefikia asilimia 88," amesema Dkt. Chacha.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: