Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, amesisitiza umuhimu wa watumishi wa (Sekta ya Ujenzi), kujengewa uwezo na ujuzi katika utekelezaji na usimamizi wa miradi inayoendelea ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
Prof. Mbarawa amesema hayo mjini Tabora, wakati akifungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Sekta hiyo ambapo pamoja na mambo mengine amesisitiza umuhimu wa wataalam wa usanifu wa barabara, madaraja na majengo kujiimarisha na kupata uzoefu ili kuboresha utendaji kazi na kupunguza gharama zinazoongezeka katika miradi kutokana na kukosewa kwa usanifu.
“Hakikisheni mnawapa ujuzi wa kutosha watalaamu wote ili waweze kuwa wabunifu, wanaojiamini na wenye uwezo mkubwa wa kusimamia miradi”, amesema Prof. Mbarawa.
Katika hatua nyingine, Waziri Prof. Mbarawa ameitaka Wizara pamoja na Wakala wa Barabara (TANROADS), kusimamia kwa karibu malalamiko katika vituo vya mizani ili kuhakikisha mizani zote nchini zinakuwa katika ubora wakati wote na kutoa huduma nzuri kwa wadau wa usafirishaji.
Amesisitiza umuhimu wa watumishi wa Sekta ya ujenzi kufanya mazoezi kila wakati ili kujiepusha na maradhi yasiyoambukizwa na hivyo kuwa na rasilimali watu kubwa yenye afya njema katika utekelezaji wa miradi.
Kwaupande wake Katibu Mkuu wa Sekta ya Ujenzi ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza hilo Balozi Eng. Aisha Amour, amemhakikisha Waziri Prof. Mbarawa kuwa watumishi wa Sekta hiyo wamejipanga kuhakikisha wanasimamia miradi yote ya ujenzi iliyopitishwa kwenye Bajeti kikamilifu na hivyo kufikia malengo yaliyopangwa na Wizara.
Balozi Aisha amesema wamejipanga kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi kwa wataalam ili kuwajengea uwezo wa kuendana na mabadiliko ya mara kwa mara ya teknolojia na hivyo kuleta tija na ufanisi mahali pa kazi.
Mkutano wa Baraza la Wafanyakazi Sekta ya Ujenzi pamoja na mambo mengine umepitisha rasimu ya bajeti ya Sekta hiyo kwa mwaka wa fedha 2022/2023.
Toa Maoni Yako:
0 comments: