Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako akiongea na washiriki wa Mkutano wa kubadilishana uzoefu kati ya Tume ya Vyuo Vikuu na Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu (hawapo pichani) wakati akifungua Mkutano huo Jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe akiongea na Washiriki wa Mkutano wa kubadilishana uzoefu kati ya Tume ya Vyuo Vikuu na Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu (hawapo pichani) wakati wa ufunguzi wa Mkutano huo Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya washiriki wa Mkutano wa kubadilishana uzoefu kati ya Tume ya Vyuo Vikuu na Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu wakimsikiliza Mgeni Rasmi, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mhe. Prof Joyce Ndalichako (hayupo pichani).

WAZIRI wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako amewataka Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki nchini kusimamia kikamilifu uendeshaji wa Vyuo vyao ili kuhakikisha wanapunguza changamoto zilizopo.

Ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa kubadilishana uzoefu kati ya Tume ya Vyuo Vikuu (TCU) na Wenyeviti wa Mabaraza ya Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki ambapo amesisitiza umuhimu wa kuimarisha mifumo ya usimamizi na uendeshaji wa vyuo hivyo ili kufikia lengo hilo.

Ametaja baadhi ya changamoto hizo kuwa ni upungufu wa wahadhiri wenye sifa stahiki, kutolipa wafanyakazi mishahara na stahiki nyingine, kuwepo kwa miundombinu ya kufundishia na kujifunzia isiyokidhi viwango pamoja na ucheleweshaji wa matokeo ya mitihani.

"Kuna baadhi ya vyuo haviwalipi wafanyakazi hadi inapelekea wao kushikilia karatasi za mitihani ya wanafunzi na hivyo kuwanyima wanafunzi haki ya kupata matokeo yao kwa wakati. Hii si sawa kwa kuwa tunakuwa tunawaandaa wahitimu ambao wanatoka chuoni wakiwa na hasira na hivyo baadae kupata watendaji wasio na maadili bora," amesisitiza Waziri Ndalichako.

Katika hatua nyingine, Waziri Ndalichako amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha upatikanaji wa mkopo nafuu wa zaidi ya Shilingi bilioni 972 kutoka Benki ya Dunia utakaotumika kuimarisha Elimu ya Juu ambapo jumla ya Vyuo 14 vitanufaika na kupunguza changamoto ikiwemo ya miundombinu.

"Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan Mei 27 mwaka huu imesaini Mradi wenye thamani ya Dola za Kimarekani milioni 425, sawa na Shilingi bilioni 972 kwa ajili ya kuimarisha Elimu ya Juu. Haijawahi kutokea katika historia ya Nchi yetu kuweza kupata fedha nyingi kiasi hicho hivyo nimpongeze sana Rais wetu kwa kuwezesha hilo,"

Waziri Ndalichako pia ametoa maelekezo kwa Tume ya Vyuo Vikuu kuchukua hatua stahiki kwa yeyote iwe Taasisi au mtu binafsi anayekiuka taratibu zilizowekwa za maombi ya udahili kutokana na kuzuka kwa tabia ya Vyuo kutuma maombi ya udahili kwa niaba ya waombaji na kuwathibitishia (confirmation) udahili wao hali ambayo huwanyima waombaji uhuru wa kuchagua vyuo wanavyovipenda.

Naye Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof James Mdoe amesisitiza umuhimu wa Menejinenti za Vyuo Vikuu kusikiliza na kufanyia kazi malalamiko yanayotolewa na wanafunzi vyuoni badala ya kuyapuuza na hatimaye malalamiko hayo kuletwa Wizarani.

Amesema kumekuwa na malalamiko kwa baadhi ya Vyuo kuchelewa kuwapa wanafunzi fedha za mikopo na kuwataka kuteua maafisa mikopo wenye uwezo ili kupunguza malalamiko hayo.

"Baadhi ya vyuo vinachelewa kupeleka stakabadhi ya malipo Bodi ya Mikopo hadi inafika wakati wa mitihani Bodi inakuwa bado haijafanya malipo, matokeo yake vinawazuia wanafunzi kufanya mitihani au kuwafungia matokeo yao. Hii si sahihi, mnatakiwa mpeleke stakabadhi hizo kwa wakati," amefafanua Prof Mdoe.


Akiongea kwa niaba ya washiriki, Makamu Mkuu wa Chuo cha Mzumbe, Prof. Lugano Kusiluka amekiri kupokea ushauri na maelekezo na kuahidi kuyafanyia kazi ili kuboresha utendaji kazi na kupunguza malalamiko na changamoto zilizopo.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: