Na Mwandishi Wetu

MWAKILISHI wa Tanzania katika shindano la dunia (Miss World), Brigitte Alfred, amefanya kweli baada ya kufanikiwa kutwaa nafasi ya tatu katika shindano dogo la Beauty with a Purpose.

Brigitte aliye Redd’s Miss Tanzania 2012/2013, anatarajiwa kupanda jukwaani leo huko Bali, Indonesia kuwania taji la Miss World.

Taji la Beauty with a Purpose limetwaliwa na Ishani Shrestha wa Nepal na kilichomfanya Brigitte ashike nafasi hiyo ni kutokana na video aliyoiwasilisha kuhusu kazi alizofanya kwa jamii hapa nchini.

Video aliyoiwasilisha Brigitte ilionyesha kazi ya jamii aliyoifanya kuwasaidia watu wenye ulemavu wa ngozi.

Nafasi ya pili ilichukuliwa Erin Holland wa Australia, huku lile la ‘Top Model’ likitwaliwa na Megan Young wa Ufilipino, Jacqueline Steenbeek wa Uholanzi akatwaa la michezo, Sancler Frantz wa Brazil akachukua la ‘Beach Fashion’, Vania Larissa wa Indonesia alitwaa la Miss World Talent na Navneet Dhillon wa India akatwaa la Multimedia.

Washindi watano katika mashindano hayo madogo wana uhakika wa kuingia hatua inayofuata, huku Brigitte kwa nafasi hiyo ikiwa imemsaidia kwa kiwango kikubwa kujiamini kwa kusonga mbele.

Brigitte anashiriki fainali leo, huku akiwa na kazi kubwa ya kuhakikisha anafuata nyayo za Nancy Sumari aliyefanikiwa kutwaa taji la Afrika katika mashindano ya Miss World ya mwaka 2005.

Akizungumza kutoka Indonesia, Brigitte alisema, wengi walifurahi kazi yake aliyopeleka ambayo ilionyesha pia kwa kiasi kikubwa jinsi watu wenye ulemavu wa ngozi wanavyohitaji msaada, hasa kutokana na kuwindwa na baadhi ya watu.

“Waliipenda kazi yangu, lakini kwa shindano la kesho (leo) nina uhakika mkubwa wa kufanya vizuri, kwani vigezo vyote ninavyo na nimejiandaa kwa muda mrefu mno.

“Niseme wazi nimejiandaa kwa muda mrefu mno na nashukuru wote walionisaidia kwa njia moja au nyingine na hii inanipa moyo wa kufanya vizuri zaidi,” alisema.

Wakati akimuaga Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara, alimtaka ahakikishe anaipeperusha vizuri bendera ya Tanzania na kufanya vyema katika mashindano hayo.

“Fahamu fika kwamba unakwenda Indonesia kama Miss Tanzania na si Brigitte, hivyo unatuwakilisha Watanzania wote, sisi tuko nyuma yako unachotakiwa ni kujiamini tu na utafanikiwa.”

Mrembo huyo alifanikiwa kulitwaa taji la Redd’s Miss Tanzania mwishoni mwa mwaka jana, akitokea kitongoji cha Sinza na Kanda ya Kinondoni.

Taji la Miss World linashikiliwa na mrembo Wenxia Yu kutoka China, ambaye tayari alikuwa Indonesia kwa ajili ya kulivua taji hilo.

Redd’s Miss Tanzania kwa sasa inadhaminiwa na kinywaji cha Redd’s Original kinachozalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL).
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: