MGAWO wa umeme unaoendelea nchini hivi sasa umepungua hasa katika Jiji la Dar es Salaam, kutokana na kuongezeka kwa uzalishaji katika mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Independent Power Tanzania Limited (IPTL). 

Kwa zaidi ya siku tatu hali ya mgawo katika maeneo mbalimbali ya Dar es Salaam yameonyesha unafuu wa kupata umeme kwa siku nzima huku mengine yakipata mgawo kidogo. 

Akizungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu jana, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Philip Saliboko, alisema uzalishaji wa mitambo hiyo umeongezeka tangu kati kati ya wiki iliyopita. 

“Uzalishaji katika mitambo ya IPTL umeongezeka tangu siku tano zilizopita, kwa sasa tunazalisha megawati 100 na hali hiyo inatokana na serikali kununua mafuta mazito ya kuendeshea mitambo hii,” alisema mtendaji huyo wa Rita ambaye kampuni yake ni Mfilisi wa Kampuni ya IPTL. 

Kabla ya uzalishaji wa IPTL kuongezeka, mitambo hiyo ilikuwa ikizalisha megawati 10 pekee za umeme. Kwa mujibu wa Saliboko, kupungua kwa mgawo huo kunatokana na IPTL kuongeza uzalishaji na kwamba jinsi siku zitakavyokwenda ndivyo hali itakavyozidi kuwa nzuri kwa nchi nzima ikitegemeana pia na kunyesha kwa mvua. Aliwataka wananchi kuendelea kuvuta subira na kuwa na imani na utendaji wao na serikali kwa ujumla. 

Katika hatua nyingine, baadhi ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wamepongeza hatua ya mgawo kupungua hivyo kuitaka serikali kutimiza ahadi inazowaahidi ili kumaliza kabisa mgawo. Salim Ahmed, mkazi wa mbagala alisema hakuamini baada ya kuona tangu juzi nyumbani kwake kukiwa na umeme kwa siku nzima na kwamba kama mgawo umemalizika ni furaha kwake. 

Naye Flora Amon wa Buguruni, alisema pamoja na kupungua kwa mgawo serikali haina budi kutafuta mbinu mbadala za kutatua matatizo yanayosababisha mgawo. Naye Khalfan Abdulah alisema serikali haina budi kuwa makini na mambo mbalimbali yahusuyo maendeleo ya nchi hasa tatizo la umeme. Hatua ya IPTL kuongeza uzalishaji imetokana na serikali kupitia Waziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, kuahidi kwa jamii kama njia ya kupunguza mgawo. 

Kwa mujibu wa Ngeleja ambaye alitoa kauli hiyo mjini Dodoma hivi karibuni wakati akizungumza na waandishi wa habari, hatua hiyo itatokana na Hazina (Wizara ya Fedha) kutoa fedha za kununua mafuta mazito ya kuendesha mitambo hiyo. Naye Tumaini Steven mkazi wa Mtoni Kijichi alisema tangu Jumamosi wakazi wa huko wamekuwa wakipata umeme kwa siku nzima na kwamba anapongeza juhudi zilizofanywa na serikali. 

Naye Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema (CHADEMA) amewataka wananchi kuwa wavumilivu wakisubiri serikali ipatie ufumbuzi suala la mgawo wa umeme unaondelea nchini ambao Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ameahidi utamalizika Agosti 30, mwaka huu. 

Lema alisema endapo muda huo utaisha bila tatizo hilo kumalizika hatakuwa na pingamizi kwa wananchi hao kuingia barabarani kufanya maandamano kushinikiza kupatikana kwa nishati hiyo aliyodai kuwa kukosekana kwake mbali ya uchumi wa nchi kuyumba lakini linaongeza kasi ya vijana kuondolewa kwenye ajira. 

Aliyasema hayo juzi alipokuwa akifafanua hatua yake ya kukwepa kupokelewa kwa maandamano yaliyoandaliwa na madereva wa daladala mwishoni mwa wiki katika eneo la Kisongo kwa lengo la kumpokea akitokea mjini Dodoma anakohudhuria vikao vya Bunge la bajeti ambayo yalikuwa yaishie kwenye viwanja vya NMC. 

Lema alisema kuwa leo atakutana na madereva wa magari madogo ya abiria maarufu kama vifodi kusikiliza kero zao kama alivyowaahidi wiki iliyopita alipowasiliana nao akiwaomba kuacha mgomo wao uliodumu kwa siku tatu mfululizo ili wananchi wasiendelee kuteseka. 

Alisema kwa kuwa serikali imeonyesha nia ya kusikiliza kero za madereva hao na wako tayari kuzipatia ufumbuzi aliona hakuna sababu ya kuandamana na yeye kama mwakilishi wa wananchi wa Arusha Mjini ataendelea kufanya mazungumzo na serikali mpaka madereva hao wapatiwe haki zao ikiwa ni pamoja na kuacha kuonewa. 

“Nawaomba wananchi wasubiri mpaka Agosti 30 kama ahadi ya Pinda (Waziri Mkuu) haitatimia hapo tutaandamana mpaka kieleweke; hatuwezi kuadhimisha miaka 50 ya taifa huru tukiwa gizani huku serikali ikikosa sababu za msingi za kuwepo kwa tatizo hilo,” alisema Lema.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: