Articles by "HABARI"
Showing posts with label HABARI. Show all posts

Baada ya ufanisi mkubwa wa biashara kwa mwaka 2025 uliochangia kupata faida ya zaidi ya shilingi trilioni 1.04, Benki ya CRDB leo imezindua kampeni yake ya mwaka 2026 inayoitwa ‘Benki Kimpango Wako’ inayolenga kuboresha huduma kwa wateja kwa kupunguza muda wa kukamilisha muamala na kumruhusu mteja kujihudumia vile atakavyo, kwa muda wake akiwa mahali popote duniani.

Kampeni hiyo imezinduliwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela ambaye amewashukuru wateja, wawekezaji, wabia wa kimkakati pamoja na wadau wote kwa ujumla kwa imani waliyonayo kwa benki hiyo kubwa zaidi nchini.

“Mwaka jana tumepata faida kubwa kutokana na ushirikiano mkubwa tulioupata kutoka kwa wateja binafsi, wajasiriamali, taasisi, mashirika na serikali pamoja na wabia wetu. Ninyi ndiyo sababu ya uwepo wa Benki ya CRDB. Kila akaunti mliyofungua, mkopo mliouchukua, kila muamala mlioufanya, na kila mradi mlioutekeleza kupitia Benki ya CRDB vilitupa nguvu na ari ya kujituma zaidi. Ninaamini na kuomba ushirikiano huu uendelea mwaka huu pia,” amesihi Nsekela.

Mwaka 2025, Benki ya CRDB imepata faida ya shilingi trilioni 1.04 kabla ya Kodi sawa na ukuaji wa asilimia 33, huku faida baada ya kodi ikifika shilingi bilioni 725 likiwa ni ongezeko la asilimia 31 ikilinganishwa na mwaka 2024. Mizania yake nayo imeongezeka na kufika shilingi trilioni 22.2 sawa na ukuaji wa asilimia 33 na ndani ya kipindi hicho imetoa mikopo kiasi cha shilingi trilioni 13.7 sawa na ukuaji wa asilimia 32.6.
Ukuaji huo, Nsekela amesema unamaanisha uwezo mkubwa zaidi wa kufadhili miradi ya maendeleo, kusaidia kukuza mitaji ya biashara ndogo, za kati na kubwa, kuongeza uzalishaji, kutoa ajira mpya, na kuwawezesha vijana, wanawake na wajasiriamali kutimiza malengo yao ya kiuchumi.

Mafanikio haya yana akisi ushirikiano wa wadau wetu wote. Tutaendelea kutekeleza azma yetu ya kuboresha maisha ya watu wetu na uchumi wa Taifa letu pamoja na masoko mengine ambako benki yetu inatoa huduma. Sisi ni Benki Inayomsikiliza Mteja na kwa kufanya hivyo tunapata syluhisho la kila changamoto ya mteja,” amesema Nsekela.
Kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, kuongezeka kwa ushindani wa kibiashara na upangaji wa mikakati binafsi ya kiuchumi na maendeleo, Nsekela amesema wateja wanahitaji huduma za fedha ambazo ni rahisi, za haraka, na zinazoendana na mikakati waliyonayo ndio maana Benki ya CRDB imekuja na kampeni ya Benki Kimpango Wake ikikusudia na kuahidi kutoa kipaumbele kwa wateja na wadau wengine ambao ni sehemu ya mafanikio yake ya kibiashara.

Jitihada hizi za kuboresha na kuimarisha huduma kwa wateja na wadau wengine wa Benki ya CRDB, Nsekela amesema zilizanza mwaka jana pale walipofanya maboresho ya mfumo mkuu wa uendeshaji (core banking system) yakilenga kuiweka benki katika viwango vya kimataifa vya utoaji huduma na mapema mwaka huu wakazindua ofisi ya uwakilishi Dubai.
“Maboresho yetu ya mfumo mkuu wa uendeshaji wa yalilenga kubadilisha namna Benki inavyofanya kazi na jinsi mteja anavyopata huduma. Leo tunazindua kampeni tunayoiita Benki Kimpango Wako. Tunawahakikishia Watanzania na wateja wetu wengine popote duniani kuwa Benki yetu ya CRDB ni mbia wa uhakika na wa kutumainiwa katika upatikanaji wa huduma za fedha. Mwaka 2026 tunawaahidi huduma bora na za uhakika zaidi,” amesema Nsekela.

Uzinduzi wa kampeni ya Benki Kimpango Wako umefanyika katika kipindi muhimu kwa historia ya taifa wakati serikali ikianza utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayoelekeza kuwa uchumi wa Tanzania unapaswa kuwa jumuishi, wenye huduma za fedha zilizowafikia wananchi wengi zaidi, na taasisi za fedha kuwa nguzo ya ukuaji wa uchumi, ubunifu na ustawi wa jamii.
Ili kupata huduma za uhakika, wateja wanaweza kuhudumiwa katika tawi lolote la Benki ya CRDB iwe hapa Tanzania, nchini Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) au katika ofisi ya uwakilishi iliyopo Dubai au kupitia majukwaa tofauti ikiwamo Simbanking, huduma kwa njia ya intaneti au kwa CRDB Wakala. Huduma hizi zinapatikana pia hata kwa wale wanaofuata misingi ya dini kwani huhudumiwa kupitia dirisha la CRDB Al Barakah.

“Benki ya CRDB ni daraja la fursa kwa wananchi wote. Kampeni ya Benki Kimpango Wako inamkumbusha kila mdau kwamba Benki ya CRDB ni mshirika wa kutumainiwa katika safari ya maendeleo kwa mpango wa mteja katika muda wake,” amesisitiza Nsekela.
Na Mwandishi Wetu.

Tume ya Ushindani (FCC) imeweka mikakati mbalimbali ya kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi kwa wakati kwa kutumia mifumo ya kisasa katika utekelezaji wa majukumu yake, ikiwa ni sehemu ya kuongeza ufanisi na uwazi katika huduma za ushindani na biashara nchini.

Akizungumza wakati wa kikao kazi na watumishi wa Tume hiyo kilicholenga kupanga mikakati ya utekelezaji wa majukumu, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa, amesema hatua zinazochukuliwa na Tume zinalenga kuwahudumia wananchi kwa viwango vya juu vya ubora vinavyotambulika kitaifa na kimataifa.

Amesema FCC inaendelea kutekeleza dhamira ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha mazingira ya biashara nchini kwa kuwashirikisha wafanyabiashara na wananchi kupitia mifumo rafiki, ya kisasa na yenye ufanisi katika utoaji wa huduma.

Bi. Ngasongwa amebainisha kuwa katika kipindi cha siku 100 za uongozi wa Rais Samia, FCC imechukua hatua za makusudi za kusogeza huduma karibu na wananchi, ikiwemo kuanzisha Ofisi ya FCC Mkoa wa Tanga pamoja na maeneo ya mipakani, hatua iliyolenga kuongeza wigo wa huduma na kuwafikia wananchi waliopo maeneo ya pembezoni.

Ameongeza kuwa FCC imeendelea kudumisha Cheti cha Ithibati ya Ubora ISO 9001:2015 kutokana na jitihada zake za kutoa huduma kwa weledi, uwazi na kuzingatia viwango vya ubora, huku akiwapongeza watumishi kwa juhudi zao katika kulinda hadhi ya taasisi hiyo.

Katika kikao hicho, watumishi walipata fursa ya kujadili na kutoa maoni kuhusu rasimu ya Mpango Mkakati Mpya wa Tume wa miaka mitano (2026/27–2030/31), unaoakisi utekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050, sambamba na kuimarisha utamaduni wa ushirikishwaji katika maamuzi ya taasisi.

Kikao kazi hicho cha FCC kimefanyika Februari 2, 2026 katika ukumbi wa Hoteli ya Tiffany Diamond jijini Dar es Salaam.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa FCC, Bi. Khadija Ngasongwa akizungumza na watumishi wa FCC (hawapo pichani) katika kikao kazi na watumishi wa Tume, kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Tiffany Diamond, Jijini Dar es Salaam Februari 02, 2026.
Bw. Shalua Magandi, Mkurugenzi wa Huduma Saidizi akichangia mada wakati wa kikao kazi na watumishi wa Tume, kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Tiffany Diamond, Jijini Dar es Salaam Februari 02,2026.Mwenyekiti wa Tughe Tawi la FCC, Bw. Emmanuel Ndyetabula akifuatilia kikao kazi cha Kaimu Mkurugenzi Mkuu na watumishi wa Tume, kilichofanyika katika ukumbi wa Hoteli ya Tiffany Diamond, Jijini Dar es Salaam Februari 02,2026.



Sehemu ya watumishi.





Picha za pamoja.
Na Mwandishi Wetu.

Bibi Clotilda Isidory Kokupima, mkazi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, amemtembelea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, na kumuomba awasilishe shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa msaada wa Shilingi Milioni 20 uliomuwezesha kugharamia matibabu ya ugonjwa wa kansa ya utumbo uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

Akizungumza ofisini kwa Prof. Shemdoe, Bibi Clotilda alisema msaada huo wa Rais Samia ulimwezesha kupata matibabu katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam baada ya familia yake kushindwa kuendelea kugharamia matibabu kutokana na gharama kubwa, hali iliyohatarisha maisha yake.
Alieleza kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita na aliwasilisha maombi ya msaada kwa wadau zaidi ya kumi, akiwemo Mheshimiwa Rais, ambapo ndani ya mwezi mmoja alipatiwa msaada huo uliompa matumaini mapya ya kuendelea na matibabu.

Bibi Clotilda alisema fedha hizo zilimwezesha kukamilisha dozi zote za matibabu, na baada ya vipimo vya mwisho kufanyika, madaktari walithibitisha kuwa hana tena ugonjwa wa kansa ya utumbo uliokuwa ukimsumbua.
Ameongeza kuwa kwa sasa ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kila siku, huku akiendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya kila baada ya miezi mitatu kwa ushauri wa madaktari.

Kwa kumalizia, Bibi Clotilda alimshukuru Prof. Shemdoe kwa kukubali kuwasilisha shukrani zake kwa Rais Samia, akisema huruma, upendo na uongozi wa Rais umeokoa maisha yake, na kumuomba aendelee kuwasaidia wananchi wengine wenye uhitaji wa matibabu na huduma muhimu za kijamii.

Na Mwandishi Wetu, Babati – Manyara.

Maafisa Mawasiliano wa Serikali mkoani Manyara wametakiwa kujitathmini, kuimarisha weledi wao na kujipa thamani kazini ili kuongeza ufanisi wa vitengo vya mawasiliano na mchango wake katika utekelezaji wa shughuli za Serikali.

Wito huo umetolewa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Bw. Dominic Mbwette, wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili cha Maafisa Mawasiliano wa Serikali wa Mkoa wa Manyara kilichofanyika jijini Babati kuanzia Februari 2 hadi 3, 2026.

Bw. Mbwette alisema kuwa changamoto ya kutotambuliwa kwa baadhi ya Vitengo vya Mawasiliano ndani ya taasisi za Serikali inaweza kupatiwa suluhisho endapo Maafisa Mawasiliano wenyewe wataonesha kwa vitendo thamani ya taaluma yao kupitia uwajibikaji, ubunifu na matokeo chanya ya kazi wanazofanya.

“Umuhimu wenu hauamuliwi na cheo pekee bali na matokeo ya kazi zenu. Mkijipa thamani kwa kutekeleza majukumu kwa ufanisi, ni rahisi kwa viongozi na jamii kuona mchango wenu,” alisema Mbwette.

Ameongeza kuwa Maafisa Mawasiliano ni nguzo muhimu ya kuimarisha uwazi, kuwajengea wananchi uelewa wa mipango ya Serikali na kukuza imani kati ya Serikali na jamii, hivyo wanapaswa kutumia fursa hiyo kama sehemu ya kujenga taswira chanya ya utumishi wa umma.

Aidha, aliahidi kuwa Ofisi ya Katibu Tawala wa Mkoa itaendelea kutoa miongozo na maelekezo kwa Halmashauri zote ili kuhakikisha Vitengo vya Mawasiliano vinapatiwa rasilimali na bajeti stahiki kwa utekelezaji wa majukumu yao.

Kwa upande wao, Maafisa Mawasiliano walieleza kuwa kikao kazi hicho kimewapa fursa ya kubadilishana uzoefu, kuimarisha ujuzi na kuweka mikakati ya pamoja ya kuboresha utoaji wa taarifa za Serikali kwa wananchi.
Bw. Mbwette alihitimisha kwa kuwataka Maafisa Mawasiliano kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uzalendo na nidhamu ili kuimarisha uwajibikaji na uwazi katika utumishi wa umma mkoani Manyara.


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism), Bi. Shaikha Nasser Al Nowais pembezoni mwa mkutano wa Jukwaa la Serikali za Dunia (WGS2026), tarehe 3 Februari, 2026 Madinat Jumeirah, Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE). 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan akizungumza na Katibu Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii (UN Tourism), Bi. Shaikha Nasser Al Nowais pembezoni mwa mkutano wa Jukwaa la Serikali za Dunia (WGS2026), tarehe 03 Februari, 2026 Madinat Jumeirah, Dubai, Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambapo walijadili kuhusu kuimarisha ushirikiano wa Tanzania na UN Tourism katika undeshaji wa shughuli za utalii, ikiwemo utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati katika sekta hiyo nchini. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Patrobas Katambi akizungumza Kikao cha kwanza na Uongozi wa Juu wa Jeshi la Magereza, Maafisa, askari na watumishi raia(hawapo pichani),wakati wa ziara ya kwanza baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hiyo.Kikao hicho kimefanyika Makao Makuu ya Jeshi hilo,jijini Dodoma.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

Serikali imedhamiria kuimarisha kilimo na ufugaji katika Jeshi la Magereza ili kuliwezesha jeshi hilo kutumia maeneo inayomiliki kwa kilimo chenye tija huku ikiweka wazi kuyatafutia hati maeneo mbalimbali yanayomilikiwa na Jeshi hilo, lengo ikiwa kukuza kipato kwenye kilimo ikiwemo kulisha wafungwa na kufanya biashara ya mazao hayo.

Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi wakati wa Kikao cha kwanza na Uongozi wa Juu wa Jeshi la Magereza, Maafisa, askari na watumishi raia, kilichofanyika Makao Makuu ya jeshi hilo, Msalato jijini Dodoma ambapo aliambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Ayoub Mohamed Mahmoud.

“Ni jukumu letu sasa kuhakikisha maeneo yetu sasa tunayatambua mipaka yake, yale yasiyo na hati zijulikane ziko wapi na kama hazipo tutafute hati na yale yanayofaa kwa kilimo tuyainishe na tuyanakiri ili tujue tunaweza tunaweza kufanya nini.Wizara ya Mifugo na Uvuvi iko tayari kufanya kazi na sisi, Wizara ya Kilimo pia iko tayari kuhakikisha tunafanya kilimo kikubwa chenye tija na kitakachojibu haja na matamanio ya Jeshi la Magereza, lakini pia kupata kipato na kupunguza nakisi ya mahitaji, suala la upungufu wa wazabuni umelisema hapa CGP (Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza), hatuhitaji tena wazabuni kwasasa kama tutajipanga vizuri,tutawahitaji kwa hatua ya sasa lakini kwa baadae haitakuwepo kwasababu tuna magereza sehemu mbalimbali ambayo yanaweza kuzalisha mazao yanayokubali kuota sehemu husika.” Amesema Waziri Katambi

Akizungumza katika kikao hicho, Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohamed Mahmoud amesema serikali itakazia zaidi masuala ya teknolojia katika viwanda, kilimo na mifugo ili kuweza kuleta ufanisi zaidi katika utendaji wa Jeshi la Magereza ambapo aligusia dhana hiyo kuwepo katika Dira ya 2050.

Nae Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza, CGP Jeremiah Katungu amesema Jeshi linatoa mafunzo ya ujasiriamali katika Gereza la Arusha ambapo jumla ya wafungwa 209 walihitimu mwaka jana(2025), Chuo cha Uhasibu Arusha ambapo pia ameweka wazi mahusiano ya Jeshi la Magereza na Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA) huku jumla ya wafungwa 201 walihitimu mafunzo na kupewa vyeti na mamlaka hiyo.
Mtaalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Mbeleye David akizungumza na wateja wanaofika kuuza dhahabu zao.

Na Mwandishi Wetu, Singida.

Wadau wa sekta ya madini wakiwemo wachimbaji, wachenjuaji na wafanyabiashara wa madini mkoani Singida wamepongeza uwepo wa Soko la Madini Singida, wakisema limeleta mapinduzi makubwa katika biashara ya madini kwa kuimarisha uwazi, haki na ufanisi kupitia matumizi ya mfumo wa bei elekezi za kidigitali.

Akizungumza katika soko hilo, Mtaalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Mbeleye David, amesema kuanzishwa kwa soko hilo kumeleta tija kubwa kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini kwa kuweka mifumo inayowalinda dhidi ya udanganyifu wa ubora wa dhahabu na unyonyaji wa bei.

Amesema kabla ya kuanzishwa kwa masoko ya madini, mkoa wa Singida ulikuwa unaratibu kiasi kidogo cha uzalishaji, kati ya gramu 100 hadi 200 pekee, lakini kwa sasa kupitia masoko hayo umefanikiwa kuratibu uzalishaji unaoanzia kilo 50 hadi 60 kwa wachimbaji wadogo, hali inayoonesha ongezeko la ufanisi na imani ya wadau katika mfumo huo.

David ameeleza kuwa Serikali imeweka mfumo madhubuti wa bei elekezi unaolenga kumlinda mchimbaji mdogo dhidi ya kupunjwa kwa kuuza madini kwa bei duni.

Amesema soko hilo limewekewa mashine ya kisasa ya X-Ray Fluorescence (XRF) kwa ajili ya kupima ubora wa dhahabu, hatua inayohakikisha madini yanauzwa kwa kuzingatia viwango sahihi vya ubora na thamani halisi.

Ameongeza kuwa, tofauti na awali ambapo bei elekezi ilitolewa kwa dhahabu ghafi pekee, kwa sasa soko linatumia ubao wa kidigitali unaoonesha bei elekezi za madini mbalimbali ikiwemo dhahabu, shaba na fedha, jambo lililoongeza uwazi na kuondoa mianya ya udanganyifu katika biashara ya madini.

“Teknolojia hii imeongeza uwazi na kurahisisha shughuli za masoko ikiwemo uthaminishaji wa madini na utoaji wa vibali vya kusafirisha madini ndani na nje ya nchi, ambazo sasa zinafanyika kwa wepesi na kwa haraka zaidi,” amesema David.

Kwa upande wake, mfanyabiashara wa madini, Abubakari Omary, amesema pamoja na mafanikio yaliyopo, elimu kuhusu matumizi ya bei elekezi inapaswa kuendelea kutolewa kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili kuepusha sintofahamu na migogoro wakati wa kufanya biashara.

“Elimu ni msingi muhimu ili kila mdau aelewe haki na wajibu wake na kufanya biashara kwa kuzingatia bei halisi ya soko,” amesema Omary.

Aidha, wadau wamepongeza mfumo mpya wa masoko ya madini unaowawezesha wachimbaji wasio na leseni kujisajili na kuuza madini yao moja kwa moja katika masoko ya madini bila kulazimika kutumia leseni ya mfanyabiashara, hatua ambayo imeondoa kikwazo kikubwa kilichokuwepo awali.

Kwa ujumla, uwepo wa Soko la Madini Singida umetajwa kuwa kichocheo muhimu cha maendeleo ya sekta ya madini mkoani humo, kwa kuongeza uwazi na usalama wa biashara, pamoja na kuongeza mapato ya serikali kupitia kudhibiti na kuzuia utoroshaji wa madini.

Mtaalam kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Singida, Mjiolojia Mbeleye David, amesema kuanzishwa kwa soko hilo kumeleta tija kubwa kwa wachimbaji wadogo na wafanyabiashara wa madini kwa kuweka mifumo inayowalinda dhidi ya udanganyifu wa ubora wa dhahabu na unyonyaji wa bei.

Mfanyabiashara wa madini, Abubakari Omary, amesema pamoja na mafanikio yaliyopo, elimu kuhusu matumizi ya bei elekezi inapaswa kuendelea kutolewa kwa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili kuepusha sintofahamu na migogoro wakati wa kufanya biashara.
Bi. Reticia Seni kutoka kampuni ya Dealer Ofisi ya Nganyila Lyapi Sweki, akihudumia wateja (hawapo pichani), waliokwenda kuuza dhahabu zao sokoni.
Madini ya dhahabu yakipimwa kwenye mizani ya kielektroniki ili kujua uzito wake.
Na Sixmund Begashe, Dodoma

DODOMA: Serikali imewataka wadau wa uwindaji wenyeji na bucha za nyamapori kuendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maliasili na Utalii ili kuimarisha mchango wa sekta ya Maliasili na Utalii katika uchumi wa taifa na kuhakikisha manufaa yake yanawafikia Watanzania kwa upana zaidi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, wakati wa kikao kilichofanyika jijini Dodoma kati ya Wizara hiyo na wadau wa sekta ya uwindaji wenyeji pamoja na bucha za nyamapori, kilicholenga kujenga uelewa wa pamoja kuhusu nafasi ya sekta hizo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
Dkt. Kijaji amesema Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuhakikisha rasilimali za maliasili zinasimamiwa kwa uwazi na uwajibikaji ili ziwe chachu ya ajira, uwekezaji na ustawi wa wananchi.

Ameeleza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi katika kusimamia na kuendeleza urithi wa maliasili, huku akisisitiza kuwa haitamvumilia mtumishi yeyote atakayekwaza juhudi za Serikali za kukuza sekta hiyo na kuwakwamisha wananchi kunufaika na fursa zilizopo.
Aidha, amewapongeza wadau hao kwa uzalendo wao na mchango wao katika uchumi, akiwataka kuendelea kushikamana na Wizara ili kufungua fursa zaidi za uwekezaji na ajira, hususan kwa vijana, kupitia sekta ya Maliasili na Utalii.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Utalii, Bw. Nkoba Mabula, amesema ofisi yake itasimamia kwa karibu utekelezaji wa maelekezo yote yaliyotolewa na Waziri, ili kuhakikisha sekta hiyo inaendelea kukua na kutoa matokeo chanya kwa taifa na wananchi.

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.

UCHAFUZI wa mazingira ya bahari, unaochangiwa kwa kiasi kikubwa na utupaji holela wa taka ngumu hususan chupa za plastiki katika mito na mitaro, umetajwa kuwa tishio kwa afya za binadamu, uhai wa viumbe wa baharini pamoja na sekta ya utalii jijini Dar es Salaam.

Hayo yameelezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Bw. Edward Mpogolo, wakati wa zoezi la usafi katika Fukwe ya Dengu iliyopo Bahari ya Hindi, lililolenga kuhamasisha usafi wa mazingira na kulinda fukwe za Jiji la Dar es Salaam.

Bw. Mpogolo amesema taka zinazotupwa ovyo katika maeneo ya makazi na mitaro huishia baharini kupitia mkondo wa maji, hali inayosababisha uchafuzi mkubwa wa fukwe na kuathiri moja kwa moja afya za wananchi pamoja na mazingira ya bahari.
Amesisitiza kuwa Serikali haitavumilia vitendo vya uchafuzi wa mazingira, na kutoa onyo kali kwa wananchi wanaoendelea kujihusisha na tabia ya utupaji holela wa taka, akibainisha kuwa sheria na kanuni za mazingira zitatekelezwa kikamilifu dhidi ya watakaobainika kukiuka.

Zoezi hilo la usafi limeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la LASDGs na JUZA, mashirika yanayojishughulisha na uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa taka ngumu jijini Dar es Salaam. Kupitia zoezi hilo, wananchi wamehamasishwa kubadilisha mtazamo wao na kuwa sehemu ya suluhisho la kulinda mazingira yao.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa JUZA, Bw. Nassib Kitabu, amesema juhudi za pamoja kati ya Serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na wananchi ndizo nguzo kuu ya kuhakikisha mazingira ya bahari na fukwe yanabaki salama na safi kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Bw. Mpogolo ameongeza kuwa Serikali ina mkakati wa kuboresha usafi katika fukwe zote za Jiji la Dar es Salaam ili kuvutia watalii wa ndani na nje ya nchi, hatua itakayochochea ukuaji wa uchumi na kuongeza fursa za ajira kwa wananchi.

Wadau wa mazingira, akiwemo Dkt. Erick Mwate na Bi. Mariam Lulida, wamepongeza hatua zinazochukuliwa na Serikali pamoja na mashirika ya kiraia katika kulinda fukwe, wakisisitiza kuwa ushiriki wa wananchi ni muhimu katika kufanikisha juhudi hizo.

Wamesema kulinda mazingira ya bahari si jukumu la Serikali pekee, bali ni wajibu wa kila mwananchi kuhakikisha fukwe na vyanzo vya maji vinabaki salama, safi na endelevu kwa manufaa ya Taifa.