Na Mwandishi Wetu.

Bibi Clotilda Isidory Kokupima, mkazi wa Wilaya ya Kasulu mkoani Kigoma, amemtembelea Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe, na kumuomba awasilishe shukrani zake kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa msaada wa Shilingi Milioni 20 uliomuwezesha kugharamia matibabu ya ugonjwa wa kansa ya utumbo uliokuwa ukimsumbua kwa muda mrefu.

Akizungumza ofisini kwa Prof. Shemdoe, Bibi Clotilda alisema msaada huo wa Rais Samia ulimwezesha kupata matibabu katika Hospitali ya Ocean Road jijini Dar es Salaam baada ya familia yake kushindwa kuendelea kugharamia matibabu kutokana na gharama kubwa, hali iliyohatarisha maisha yake.
Alieleza kuwa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa huo kwa kipindi cha zaidi ya miaka sita na aliwasilisha maombi ya msaada kwa wadau zaidi ya kumi, akiwemo Mheshimiwa Rais, ambapo ndani ya mwezi mmoja alipatiwa msaada huo uliompa matumaini mapya ya kuendelea na matibabu.

Bibi Clotilda alisema fedha hizo zilimwezesha kukamilisha dozi zote za matibabu, na baada ya vipimo vya mwisho kufanyika, madaktari walithibitisha kuwa hana tena ugonjwa wa kansa ya utumbo uliokuwa ukimsumbua.
Ameongeza kuwa kwa sasa ameruhusiwa kuendelea na shughuli zake za kila siku, huku akiendelea kufanyiwa uchunguzi wa afya kila baada ya miezi mitatu kwa ushauri wa madaktari.

Kwa kumalizia, Bibi Clotilda alimshukuru Prof. Shemdoe kwa kukubali kuwasilisha shukrani zake kwa Rais Samia, akisema huruma, upendo na uongozi wa Rais umeokoa maisha yake, na kumuomba aendelee kuwasaidia wananchi wengine wenye uhitaji wa matibabu na huduma muhimu za kijamii.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: