Na Mwandishi Wetu

Baadhi ya wachimbaji na wakazi wa eneo la Mirerani wilayani Simanjiro, mkoani Manyara, wameeleza kutoridhishwa na uamuzi wa wafanyabiashara wa eneo la Opec Machimboni kupandisha bei za bidhaa mbalimbali kwa madai ya kupanda kwa gharama za maisha.

Malalamiko hayo yameibuka baada ya kusambaa kwa tangazo linaloonyesha wafanyabiashara hao wamekutana na kukubaliana kuweka bei mpya za bidhaa mbalimbali zinazotumika na wachimbaji pamoja na wananchi wa eneo hilo.

Kwa mujibu wa tangazo hilo, baadhi ya bidhaa zilizopandishwa bei ni pamoja na maji ya kunywa, vinywaji baridi, maziwa, vocha, soda na bidhaa nyingine za matumizi ya kila siku.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya wachimbaji walisema hatua hiyo siyo sahihi kwa kuwa imefanyika kwa makubaliano ya wafanyabiashara pekee bila kuzingatia hali halisi ya uchumi wala uwezo wa watumiaji wa mwisho.

Walisema kupanda kwa bei hizo kunaongeza ugumu wa maisha kwa wachimbaji wadogo na wafanyakazi wa migodini ambao hutegemea kipato cha kila siku.

Mbali na hilo, wananchi hao pia walilalamikia nauli ya bodaboda inayotozwa ndani ya eneo tengefu la madini kutoka getini hadi Opec kufikia Sh2,000, wakidai kuwa haiendani na bei elekezi iliyotangazwa hivi karibuni na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (SUMATRA).

“Wanaoumia ni watumiaji wa mwisho. Ifike mahali wananchi wapaze sauti juu ya hali hii,” alisema mmoja wa wachimbaji aliyeomba kutotajwa jina.

Baadhi ya wananchi wamezitaka mamlaka husika kuingilia kati suala hilo kwa kufanya uchunguzi wa bei zinazotozwa na kuhakikisha kunakuwa na usimamizi wa haki kwa walaji na wafanyabiashara.

Hadi tunakwenda mitamboni, viongozi wa eneo hilo hawakuwa wametoa tamko rasmi kuhusu malalamiko hayo

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: