Na Mwandishi Wetu, Arusha
Uzinduzi huo umefanyika katika Kata ya Terrat na kuhudhuriwa na mamia ya wananchi waliopata fursa ya kujifunza na kuelimishwa kuhusu upatikanaji wa mikopo, uwekezaji pamoja na usimamizi bora wa fedha.
Akizungumza katika hafla hiyo, Afisa Maendeleo wa Jiji la Arusha, Shabani Manyama, aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Jiji, amesema halmashauri imetenga zaidi ya Sh bilioni 5.3 kwa ajili ya mikopo kwa wananchi katika robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Manyama alisema fedha hizo zipo tayari kutolewa, hivyo wananchi wanapaswa kutumia nafasi hiyo kujikwamua kiuchumi na kuboresha maisha yao kupitia shughuli mbalimbali za uzalishaji.
Aidha, aliwataka wananchi kuwa makini wanapochukua mikopo kwa kuhakikisha wanakuwa na malengo mahsusi, kufanya tathmini ya biashara zao na kutumia fedha hizo kwa kazi iliyokusudiwa.
“Mkopo si fedha ya matumizi holela, bali ni nyenzo ya kukuza uchumi wa mtu binafsi na jamii kwa ujumla,” alisema Manyama.
Miongoni mwa wananchi walioshiriki uzinduzi huo, Elizabeth Shirima alisema fursa hizo zimekuja kwa wakati muafaka na zina matumaini ya kuwasaidia wananchi wengi kujikwamua kimaisha.
Alisema utoaji wa mikopo yenye masharti nafuu utawapa nafasi wananchi wengi zaidi kushiriki katika shughuli za maendeleo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Ilaitairo, Kata ya Terrat, Aron Lukumai, alisema wananchi wamepokea kwa furaha ujio wa fursa hizo, akieleza kuwa changamoto kubwa iliyokuwepo awali ilikuwa ni ukosefu wa taarifa na uelewa.
Aliongeza kuwa kusogezwa kwa huduma karibu na wananchi kutarahisisha upatikanaji wa mikopo na kuongeza ushiriki wa wananchi katika shughuli za kiuchumi.
Kwa ujumla, zoezi hilo limepokelewa kwa mwitikio chanya na linatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi wa Jiji la Arusha kupitia matumizi sahihi ya fursa zinazotolewa.











Toa Maoni Yako:
0 comments: