Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, amefanya mabadiliko mapya katika baadhi ya nafasi za uongozi ndani ya Serikali, huku akiteua viongozi watatu kushika nyadhifa muhimu Ikulu na kwenye masuala ya kidiplomasia.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi leo, Novemba 19, 2025, aliyesainiwa na Balozi Dkt. Moses M. Kusiluka, uteuzi huo umehusisha viongozi wafuatao:

Kwanza, Mhe. Rais amemteua Bw. Tido Mhando kuwa Mshauri wa Rais, Habari na Mawasiliano, nafasi ambayo inatarajiwa kuongeza nguvu katika kuratibu taarifa za Serikali na kuimarisha mawasiliano ya Ikulu.

Pili, Bw. Bakari Steven Machumu ameteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, akichukua nafasi ya Bi. Sharifa Bakari Nyanga ambaye amepangiwa majukumu mengine. Machumu anachukuliwa kuwa miongoni mwa wataalamu wenye uzoefu mpana katika masuala ya habari na mawasiliano ya kimkakati.

Katika hatua nyingine, Bw. Lazaro Samuel Nyalandu ameteuliwa kuwa Balozi, uteuzi unaotarajiwa kumuwezesha kulitumikia Taifa katika ngazi ya kimataifa kupitia majukumu ya kidiplomasia.

Uteuzi huu unaendelea kuashiria dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita kuimarisha mifumo ya uongozi, mawasiliano na diplomasia ya kimataifa, sambamba na kuongeza ufanisi katika kusimamia ajenda za kitaifa na kimataifa.

Taarifa hiyo imetolewa rasmi na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: