Na Mwandishi Wetu, Mwanza.

Viongozi wa dini mbalimbali mkoani Mwanza wamewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa amani, upendo na utulivu katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.

Wakizungumza kwenye Kongamano la Amani la Viongozi wa Dini, viongozi hao walisema amani ni tunu muhimu ambayo Tanzania imeilinda kwa zaidi ya miaka 60, na kwamba kila raia ana wajibu wa kuithamini na kuilinda wakati huu wa uchaguzi.

Akiwasoma tamko la Kamati ya Amani ya Mkoa wa Mwanza, Mwenyekiti Mwenza, Askofu Dk. Charles Sekelwa, alisema viongozi wa dini wataendelea kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kwa amani.

“Tunawahimiza wananchi wapige kura kwa upendo, usawa na uwazi, kisha warejee majumbani kwao kwa amani. Tutaendelea kuiombea nchi yetu ibaki na utulivu,” alisema.

Sheikh Hassan Kabeke, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, alisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa haki na maendeleo.

“Haki haiwezi kusimama bila amani. Tujitokeze kupiga kura; kuacha kupiga kura ni kujinyima haki,” alisema.

Kwa upande wake, Sheikh Amani Mussa Maumba wa Wilaya ya Nyamagana, alisema viongozi wa dini wataendelea kuhimiza amani na utulivu wakati wote wa uchaguzi.

“Baada ya kupiga kura, turudi majumbani na tusubiri matokeo kwa amani,” alisema.

Askofu Zefania Ntuza wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Victoria Nyanza aliwataka viongozi wa dini na waumini kujitokeza kupiga kura na kuwa walinzi wa amani.

Mchungaji Upendo Isaya alisisitiza kuwa maamuzi ya busara yanafanyika katika mazingira ya amani, huku Amina Masenza, Mwenyekiti wa Kamati ya Kinamama Waislamu Mkoa wa Mwanza, akiwataka wanawake kushiriki uchaguzi ili kulinda haki na amani ya nchi.
Akihitimisha kongamano hilo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwahakikishia wananchi kuwa serikali na vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu.

“Wananchi wajitokeze kupiga kura bila hofu. Serikali ipo kazini kuhakikisha usalama na amani vinatawala,” alisema Mtanda.

Kongamano hilo lilihudhuriwa na viongozi wa madhehebu mbalimbali, vijana na wadau wa amani, waliotoa wito uchaguzi ufanyike kwa haki, upendo na mshikamano kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: