
Na Mwandishi Wetu, Arusha.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na mageuzi katika sekta ya usafiri wa umma baada ya kuvunja Bodi za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) na Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), na kuteua viongozi wapya katika nafasi mbalimbali za uongozi wa taasisi hizo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Dkt. Moses Kusiluka, walioteuliwa kushika nafasi hizo ni:
(i) Bw. David Zacharia Kafulila, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART).
(ii) Balozi Dkt. Ramadhani Kitwana Dau, Mwenyekiti wa Bodi ya Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART).
(iii) Bw. Said Habibu Tunda, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART), akichukua nafasi ya Dkt. Athumani Kihamia ambaye uteuzi wake umetenguliwa.
(iv) Bw. Pius Andrew Ng’ingo, Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mabasi Yaendayo Haraka (UDART), akichukua nafasi ya Bw. Waziri Kindamba ambaye uteuzi wake pia umetenguliwa.
Hatua hii ya Rais Samia inatajwa kuwa ni sehemu ya mkakati wa kuhakikisha huduma ya usafiri wa mwendokasi inaboresha zaidi, kuondoa changamoto zilizokuwapo ikiwemo msongamano wa abiria, ucheleweshaji wa mabasi na upungufu wa vyombo vya usafiri.
Aidha, uteuzi huu unafuatia malalamiko ya muda mrefu kutoka kwa wananchi kuhusu upungufu wa huduma ya mabasi ya mwendokasi, ambapo hivi karibuni Serikali iliongeza idadi ya mabasi ili kupunguza kero kwa wakazi wa Dar es Salaam.
Taarifa hiyo imetiwa saini na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Bi. Sharifa B. Nyanga.


Toa Maoni Yako:
0 comments: