Dar es Salaam, Oktoba 8, 2025: Kuanzia Oktoba 23, 2025, Tanzania itaunganishwa na nchi nyingine sita za Afrika ambazo raia wake watalazimika kulipa dhamana kubwa ya kifedha ili kupata viza za Marekani za biashara (B-1) na utalii (B-2).
Kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani, kiwango cha dhamana hiyo kitaanzia kati ya dola 5,000 (takribani shilingi milioni 12 za Tanzania) hadi dola 15,000 (takribani shilingi milioni 37). Fedha hizo zitalipwa kabla ya kupewa viza na zitarejeshwa endapo mwombaji atazingatia masharti ya viza yake na kuondoka Marekani kwa wakati.
Hatua hiyo imechukuliwa kutokana na ripoti zinazoonyesha baadhi ya raia kutoka nchi husika, wakiwemo Watanzania, wamekuwa wakipita muda wa viza zao pindi wanapokuwa Marekani.
Mbali na Tanzania, nchi zingine za Afrika zilizoorodheshwa ni pamoja na Mali, Mauritania, Sao Tome and Principe, Gambia, Malawi na Zambia.
Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki imethibitisha kuwa tayari imeanza mazungumzo ya kidiplomasia na Marekani ili kupata ufumbuzi wa changamoto hii. Serikali imeeleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na Marekani ni wa muda mrefu na umejengwa katika misingi ya urafiki, hivyo jitihada zinafanyika kuhakikisha hatua hiyo haiathiri ushirikiano wa pande mbili.
Aidha, serikali imewahakikishia Watanzania kuwa agizo hilo halihusishi aina zote za viza, bali linahusu tu wale wanaoomba viza za muda mfupi kwa biashara na utalii. Wananchi wametakiwa kuendelea kufuata taratibu rasmi za maombi kupitia Ubalozi wa Marekani.


%20(3).jpeg)
Toa Maoni Yako:
0 comments: