Na Mwandishi Wetu, Kahama.
Watoa huduma za vinyozi katika Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, wameadhimisha Siku ya Vinyozi Duniani kwa kufanya matembezi ya amani na shughuli za usafi katika Hospitali ya Manispaa ya Kahama.
Akizungumza baada ya zoezi hilo jana Septemba 16, 2025, Mwanasheria wa Manispaa hiyo, Steven Magala, akimwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Mhe. Frank Nkinda, alisema serikali inatambua mchango mkubwa wa sekta ya vinyozi, ikibainisha kuwa ni chanzo muhimu cha ajira kwa vijana wengi.
“Serikali ipo bega kwa bega na ninyi. Tunatambua mchango wenu siyo tu katika kutoa ajira bali pia katika kukuza uchumi. Ni vyema mkashirikiana kupitia umoja wenu ili sekta hii iendelee kukua,” alisema Magala.
Kwa upande wake, Katibu wa Umoja wa Vinyozi Wilaya ya Kahama, Juma Diwani, alisema maadhimisho hayo yalianza na matembezi ya amani kama njia ya kufikisha ujumbe kwa jamii kuhusu mchango wa kada hiyo, sambamba na kufanya usafi kama sehemu ya kudumisha afya na mazingira bora.
Maadhimisho hayo yaliyoongozwa na kaulimbiu isemayo “Sekta ya Vinyozi ni Injini ya Ajira kwa Vijana, Shiriki Uchaguzi Mkuu”, yalilenga pia kuhamasisha vijana kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii na kitaifa.
Siku ya Vinyozi Duniani huadhimishwa kila mwaka Septemba 16, ambapo wadau wa sekta hiyo hutumia nafasi hiyo kuonyesha mshikamano na mchango wao kwa jamii.






















Toa Maoni Yako:
0 comments: