Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) ofisi ya Zanzibar, Mhe. Khatib Mwinyichande, ametoa wito kwa wanasiasa nchini kuhakikisha wanaweka mbele maslahi ya wananchi na kuzingatia amani kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Akizungumza mara baada ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) kuzindua rasmi kampeni za vyama vya siasa Septemba 12, 2025, Kamishna Mwinyichande alisema viongozi wa kisiasa wanapaswa kuwa makini na kauli wanazotoa majukwaani ili kuepuka kuchochea fujo na uvunjifu wa amani.
“Kiongozi anaweza kusema jambo kwa maslahi yake ya uchaguzi, lakini maneno yake yakawaathiri wananchi wengi na kusababisha uvunjifu wa amani. Tume inawasihi viongozi wa siasa wazingatie maslahi ya watu wengi hasa wanapozungumza, ili kuimarisha amani iliyopo,” alisema.
Aidha, aliwakumbusha wanasiasa kuwa mikutano ya kampeni huhudhuriwa na watu wa makundi mbalimbali wakiwemo wazee, watoto na wasiojiweza, hivyo ni wajibu wa viongozi kulinda usalama wao badala ya kuwatia hatarini kwa kauli au vitendo vya vurugu.
“Wanasiasa wanapoanzisha fujo kwenye majukwaa kwa maslahi ya vyama vyao, wanawaathiri wananchi wengi wanaowazunguka. Hali hiyo ni kinyume cha misingi ya utawala bora na viongozi wa aina hiyo hawafai katika jamii,” alisisitiza Kamishna Mwinyichande.
THBUB imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa kampeni na kutoa elimu ya haki za binadamu ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika katika mazingira ya haki, amani na usalama kwa wote.



Toa Maoni Yako:
0 comments: