Dar es Salaam, Septemba 2, 2025 — Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imetangaza kuwa Sheria ya Fedha ya mwaka 2025, ambayo ilianza kutumika Julai 1 mwaka huu, imefanyia marekebisho Kifungu cha 5 cha Sheria ya VAT Sura ya 148 kwa kupunguza kiwango cha kawaida cha Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) kutoka asilimia 18 hadi asilimia 16.

Hata hivyo, TRA imefafanua kuwa utekelezaji rasmi wa punguzo hilo la VAT unategemea tangazo la umma litakalotolewa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, ambalo litaainisha watu na makundi yatakayostahili punguzo hilo pamoja na utaratibu utakaotumika.

Kamishna Mkuu wa TRA, Bw. Yusuph Juma Mwenda, amesema kwa sasa mamlaka inaendelea na maandalizi ya kiufundi na kisheria kuhakikisha kuwa utekelezaji wa punguzo hilo unafanyika kwa mujibu wa sheria. Aliongeza kuwa mara baada ya maandalizi hayo kukamilika, wananchi watajulishwa rasmi jinsi ya kunufaika na punguzo hilo la VAT.

“Tunatambua umuhimu wa utekelezaji wa punguzo hili kwa wananchi na wafanyabiashara. Mara baada ya taratibu kukamilika, taarifa rasmi itatolewa ili kila mmoja afahamu namna ya kunufaika,” amesema Bw. Mwenda.

Kwa mujibu wa TRA, hatua hii inalenga kupunguza gharama za bidhaa na huduma kwa wananchi, sambamba na kuunga mkono juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya biashara na kuongeza ustawi wa Taifa.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: