
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, ameagiza kuanzia sasa mabaunsa wasitumike tena kuwaondoa watu kwenye nyumba zenye migogoro, badala yake kazi hiyo ifanywe na madalali wa mahakama kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi ambalo lina weledi na utaalamu wa kisheria.
Agizo hilo amelitoa leo, Septemba 24, alipofika katika kiwanja namba 891 kilichopo Msasani Beach, nyumba ambayo ipo katika mgogoro kati ya Bi. Alice Paskali Haule – mke wa marehemu Justis Lugaibula – na Bwana Muhamed Mustafa Yusufali, ambaye anadaiwa alinunua nyumba hiyo kutoka kwa marehemu bila kumshirikisha mkewe.
Agizo la Chalamila limekuja baada ya kusambaa video zikionyesha mabaunsa wakitumia nguvu kubwa na vitendo vya ukiukwaji wa haki za binadamu walipokuwa wakiwaondoa wapangaji na wakazi wa nyumba hiyo Septemba 23.

.jpeg)
“Kuanzia sasa sitaki kusikia mabaunsa wanatumika tena kuwaondoa watu kwenye nyumba zenye migogoro. Madalali wa mahakama wanapaswa kushirikiana na Jeshi la Polisi, ambalo lina weledi wa kufanya kazi hii kwa mujibu wa sheria,” amesema RC Chalamila.
Aidha, RC huyo ameagiza nyumba hiyo kutotumika na upande wowote hadi mgogoro utakapopatiwa ufumbuzi. Amesisitiza kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, aunde kamati ya wataalamu ikiwemo Jeshi la Polisi, ofisi ya Kamishna wa Ardhi na wataalamu wengine, na kisha pande zote mbili za mgogoro kufika ofisini kwake Ijumaa, Septemba 26.

Kwa upande wake, Bi. Alice Haule amesema nyumba hiyo waliinunua na marehemu mumewe mwaka 2008, lakini amekuwa akipata usumbufu kutoka kwa mabaunsa wanaodai Yusufali alinunua nyumba hiyo. “Nilichokifahamu ni kuwa mume wangu na Yusufali walikopeshana pesa, sio kuuza nyumba,” alisema Alice.
Hata hivyo, mwakilishi wa Yusufali, Bi. Hajja Mungula, amesema ana uthibitisho kuwa nyumba hiyo ilinunuliwa mwaka 2011 kwa shilingi milioni 262 na kwamba Bi. Alice alitia alama ya dole gumba kwenye nyaraka za mauziano.
Kamishna Msaidizi wa Ardhi mkoa wa Dar es Salaam, Bw. Shukrani Kyando, amesema nyaraka zinaonyesha mara kadhaa umiliki wa nyumba hiyo ulibadilishwa na kwa sasa hati inasomeka jina la Muhamed Mustafa Yusufali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Mhe. Saad Mtambule, aliongeza kuwa changamoto kubwa imekuwa ni uwepo wa mabaunsa wasio na weledi wanaotumika katika migogoro ya ardhi, hali inayosababisha madhila kwa wananchi.


Toa Maoni Yako:
0 comments: