Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Mgombea urais kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, Luhaga Mpina, amechukua fomu ya kugombea nafasi ya urais leo, Septemba 13, 2025, katika ofisi za Tume Huru ya Uchaguzi (INEC), huku akitoa msimamo wa kipekee wa kukataa gari la kampeni aina ya Landcruiser linalotolewa na tume hiyo kwa wagombea.
Mpina amekuwa mgombea wa kwanza kati ya wagombea 17 waliojitonkeza kugombea urais kukataa usafiri huo, wakati wagombea wengine 16 tayari wamepokea magari hayo na kuanza kuyatumia kwenye kampeni zao.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fomu, Mwanasheria wa ACT-Wazalendo, Omari Said Shabani, alisema chama hicho hakina changamoto upande wa usafiri na kilichoomba kwa tume ni kuhakikisha kinalindwa kwa mujibu wa sheria za uchaguzi.
“Tunashukuru kwa ofa ya magari, lakini ACT-Wazalendo tumejipanga na tunajitosheleza kwa usafiri wa kampeni. Tunaiomba INEC ihakikishe ulinzi kwa mgombea wetu na timu yake, hilo ndilo muhimu zaidi kwetu,” alisema Shabani.
Uamuzi huo umeibua mjadala wa kisiasa, baadhi ya wachambuzi wakisema unaleta taswira ya chama chenye kujiamini, huku wengine wakitafsiri kama mkakati wa kuonesha tofauti ya ACT-Wazalendo na vyama vingine katika uchaguzi wa mwaka huu.



Toa Maoni Yako:
0 comments: