Na Mwandishi Wetu.

Dar es Salaam, Alhamisi, Agosti 21, 2025: Vyombo vya habari nchini vimetakiwa kuzingatia weledi, maadili na ukweli katika kuripoti habari za uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 ili kulinda amani, utulivu na kuimarisha demokrasia nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Dkt. Egbert Mkoko, Mhadhiri wa Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), alipokuwa akizungumza kwenye mkutano wa wadau wa sekta ya habari na utangazaji kanda ya Mashariki, uliofanyika jijini Dar es Salaam.

Dkt. Mkoko amesema vyombo vya habari ni daraja muhimu kati ya wananchi, wagombea, vyama vya siasa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC), hivyo vina wajibu wa kuhakikisha taarifa sahihi na zenye uthibitisho zinawafikia wananchi kwa wakati.

“Vyombo vya habari vikipeleka taarifa zisizo sahihi, zenye upendeleo au upotoshaji, vinaweza kusababisha uvunjifu wa amani na kuathiri haki ya wananchi kufanya maamuzi sahihi wakati wa kupiga kura,” amesema Dkt. Mkoko.

Kwa mujibu wa mwongozo uliotolewa na Idara ya Habari – MAELEZO, vyombo vya habari vinapaswa:

● Kuepuka kuripoti taarifa zenye chuki, ubaguzi, kashfa au lugha ya matusi.

● Kuhakikisha uwiano wa habari kwa vyama vyote vya siasa na wagombea.

● Kutumia mbinu za fact-checking kabla ya kuchapisha au kutangaza habari.

● Kutochapisha matokeo ya uchaguzi kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi kutangaza rasmi.

● Kuepuka kushiriki au kuunga mkono kampeni za kisiasa kwa namna yoyote.

Mwongozo huo pia umeelekeza kuwa matangazo yanayolipiwa lazima yatambulike wazi na yasichanganywe na habari, huku vyombo vya habari vikisisitizwa kutoripoti mikutano ya kampeni masaa 12 kabla ya siku ya kupiga kura.

Dkt. Mkoko amehitimisha kwa kusisitiza kuwa jukumu la vyombo vya habari katika kipindi cha uchaguzi ni kukuza demokrasia, kuchochea uwajibikaji wa kisiasa na kuhamasisha wananchi kushiriki kwa amani.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: