
Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetangaza ratiba rasmi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29, 2025, huku ikitoa mwongozo wa kina kuhusu hatua zote muhimu zitakazotangulia siku ya kupiga kura.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume hiyo, zoezi la kuchukua fomu za uteuzi wa kugombea nafasi ya Rais na Makamu wa Rais litaanza rasmi Agosti 9 na kukamilika Agosti 27, 2025. Aidha, kuanzia Agosti 14 hadi 27, wagombea wa nafasi za Ubunge na Udiwani nao wataruhusiwa kuchukua fomu za uteuzi.
Tarehe 27 Agosti 2025 saa 10 jioni, Tume itafanya uteuzi wa wagombea waliokidhi vigezo kwa nafasi zote: Rais, Makamu wa Rais, Ubunge na Udiwani.
Kampeni za Uchaguzi kwa Tanzania Bara zitafanyika kuanzia Agosti 28 hadi Oktoba 28, 2025, huku kampeni kwa upande wa Zanzibar zikiruhusiwa hadi Oktoba 27, 2025. Kupiga kura kwa mapema Zanzibar kutafanyika Oktoba 28.
Siku rasmi ya kupiga kura kwa Taifa zima itakuwa Oktoba 29, 2025, ambapo wananchi wote waliopo kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wanahimizwa kushiriki kikamilifu.
Tume imewataka wananchi wote, vyama vya siasa, wagombea na wadau wengine kuheshimu ratiba hii na kuzingatia taratibu zote za uchaguzi ili kuhakikisha uchaguzi huru, wa haki na amani unafanyika.
Kauli mbiu ya uchaguzi huu ni "Kura Yako Haki Yako, Jitokeze Kupiga Kura."


Toa Maoni Yako:
0 comments: