.jpeg)
.jpeg)
●Mabasi 100 mapya kutoka China kuwasili mwezi Septemba
●UDART yaelekezwa kuboresha huduma ili kuondoa adha kwa wananchi
●Mradi wa Kimara na Mbagala kupata wawekezaji wapya – Trans Dar na Mophat
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Dar es Salaam – Serikali kupitia Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Albert Chalamila, imetoa maelekezo ya kuboresha huduma za mabasi yaendayo haraka (DART), ikiwa ni sehemu ya juhudi za Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za usafiri katika jiji hilo.
Akizungumza katika ziara aliyoifanya leo katika Kituo cha Kimara Mwisho, Wilaya ya Ubungo, Mhe. Chalamila amesema kuwa ameshuhudia changamoto kubwa katika huduma za usafiri wa mwendokasi, hasa kutokana na uchache wa mabasi na usimamizi usioridhisha, hali inayowasababishia wananchi adha kubwa kila siku.
"Serikali ya Rais Samia ni sikivu. Tumesikia kilio cha wananchi na sasa tunachukua hatua. Hii adha haiwezi kuendelea; UDART mnapaswa kubadilika haraka," alisema Chalamila.
Katika ziara hiyo, Chalamila alitembelea pia eneo la upanuzi wa barabara ya Kimara hadi Ubungo unaosimamiwa na TANROADS, ambapo alisisitiza umuhimu wa mkandarasi kukamilisha ujenzi kwa wakati, huku akisisitiza uhitaji wa kuwepo kwa huduma za msingi kama vyoo kwenye vituo vikubwa vya usafiri.
Kwa upande wake, Meneja wa Upangaji Ratiba na Udhibiti kutoka UDART, Bw. Daniel Madilu, alieleza kuwa tayari wamefanya tathmini ya kina kuhusu changamoto zilizopo na kwamba mabasi mapya 100 yameagizwa kutoka China, yakitarajiwa kuwasili nchini mwezi Septemba mwaka huu.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa alitembelea ofisi za Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART) zilizopo Ubungo Maji, na kueleza kuwa tayari Serikali imepata wawekezaji wapya kwa ajili ya kuboresha huduma hizo. Mradi wa Kimara utatekelezwa na kampuni ya Trans Dar, huku ule wa Mbagala ukitarajiwa kutekelezwa na kampuni ya Mophat, ambao wataanza kuingiza magari yao hivi karibuni.
Mtendaji Mkuu wa DART, Dkt. Othman Kiamia, aliahidi kushughulikia changamoto zilizopo kwa uharaka, ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya mabasi, kuboresha ubora wa huduma, na kuhakikisha wananchi wanapata usafiri salama, wa haraka na wa uhakika.
"Tutahakikisha huduma ya mwendokasi inarejea katika viwango vya kimataifa kama ilivyokusudiwa awali. Serikali iko makini na sisi kama DART tutatekeleza maelekezo yote kikamilifu," alisema Dkt. Kiamia.
Hatua hizi zimepokewa kwa matumaini na wananchi, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakilalamikia foleni ndefu, mabasi machache, na ucheleweshwaji wa huduma katika mfumo wa usafiri wa mwendokasi. Serikali inaendelea kusisitiza kuwa dhamira ya Rais Samia ni kuona Dar es Salaam inakuwa na mfumo bora wa usafiri wa umma unaowawezesha wananchi kufika mahali wanapokwenda kwa wakati na kwa usalama.





.jpeg)

Toa Maoni Yako:
0 comments: