
●Idadi ya majina ya wagombea Ubunge na Udiwani sasa kuongezeka zaidi ya watatu
Marekebisho hayo yameridhiwa leo Jumamosi, Julai 26, 2025, kupitia Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CCM uliofanyika kwa njia ya mtandao, ukiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho, ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Mabadiliko Yaliyofanyika
Akiwasilisha marekebisho hayo, Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM – Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Ndugu Issa Haji Gavu, alieleza kuwa:
-
Ibara ya 105(7)(f) imeongezewa maneno: “isipokuwa kama Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa itaamua vinginevyo”, hivyo sasa Kamati Kuu inaweza kupitisha zaidi ya majina matatu ya wagombea wa Ubunge au Baraza la Wawakilishi.
-
Ibara ya 91(6)(c) kuhusu uteuzi wa wagombea wa Udiwani imeboreshwa kwa mtiririko huo, ikiwawezesha kupitishwa kwa wagombea zaidi ya watatu kwa kila kata pale itakapolazimu.
Samia: Demokrasia ya Ndani ya Chama Yapewa Nafasi
Akizungumza katika mkutano huo, Rais Samia amesema hatua hiyo inalenga kuimarisha na kupanua demokrasia ndani ya chama kwa kuruhusu wanachama wengi zaidi kushiriki kikamilifu katika mchakato wa kuwania uongozi.
“Tulifanya maamuzi ya kupanua demokrasia katika kuchagua viongozi wa ngazi zote, jambo lililovutia wana-CCM wengi kuomba nafasi za uongozi. Hivyo, kubaki na wagombea watatu pekee haionekani kuwa busara tena,” alisema Rais Samia.
Ameongeza kuwa katika baadhi ya majimbo, idadi ya wanaoomba kuwania ubunge imefikia hadi wagombea 40, hali iliyoonesha kiu kubwa ya uongozi miongoni mwa wanachama wa chama hicho tawala.
“Kesho tunaanza kazi ya kuchuja majina, tutajitahidi kuingiza vijana wengi zaidi,” alibainisha Rais Samia.
Mamlaka ya Kamati Kuu Yarudishwa
Marekebisho haya pia yameirudishia Kamati Kuu ya CCM Taifa mamlaka ya kufanya uteuzi mpana zaidi wa majina ya wagombea, tofauti na utaratibu wa awali uliokuwa unailazimisha kupitisha majina matatu tu yaliyopendekezwa na Kamati za Siasa za Wilaya na Mikoa.
Hatua hii inatarajiwa kuongeza uwazi, ushindani na ushirikishwaji wa makundi mbalimbali ndani ya CCM, wakiwemo wanawake na vijana, kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa siasa, hatua hiyo inaiweka CCM katika nafasi ya kuonesha mfano wa demokrasia ya ndani ya chama, huku ikiimarisha ushiriki wa wanachama wake katika mchakato wa kuchagua viongozi wa taifa.


Toa Maoni Yako:
0 comments: