Dar es Salaam: Kundi la makampuni ya Vodacom barani Afrika (Vodacom Group) limejiunga na watoa huduma wa teknolojia ili kutengeneza fursa kwa vijana barani humo kupitia ujuzi wa kidijitali kama sehemu ya ahadi yake ya kukuza ujuzi wa kidijitali kwa kizazi kijacho cha Afrika. Kwa kushirikiana na (Amazon Web Services) AWS, Microsoft, Skillsoft na mashirika mengine, Vodacom inalenga kufungua fursa za ajira kwa vijana milioni moja ifikapo mwaka 2027 kwa kuboresha ujuzi wa kidijitali katika nchi nane za Afrika.

Vodacom Digital Skills Hub itapatikana katika nchi za Afrika Kusini, Ethiopia, Tanzania, Msumbiji, Lesotho, Misri (Talimy), Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (VodaEduc) na Kenya (Industry Digital Talent Program) ili kuwapa nguvu vijana katika kuzalisha wabunifu wa kidijitali wa baadaye, na kuwezesha jamii ya kidijitali ya Afrika huku ikitumia mifumo ya kujisomea mwenyewe (u-learning) iliyopo katika masoko husika.

Kulingana na Shirika la Kimataifa la Fedha (IFC), zaidi ya ajira 230 milioni zitahitaji ujuzi wa kidijitali barani Afrika ifikapo mwaka 2030, ambapo kwa wakati huu bara hili linakutana na pengo kubwa kati ya upatikanaji wa ujuzi wa kidijitali na mahitaji ya ujuzi huo.

"Mataifa mengi ya Afrika yanakutana na changamoto kubwa za ukosefu wa ajira, ukosefu wa usawa wa kijinsia, tofauti za kipato na upatikanaji mdogo wa elimu, huduma za afya na huduma muhimu. Changamoto hizi zinachochea dhamira yetu na kuongoza mkakati wetu wa kuungana kwa ajili ya mustakabali bora, tukitumia teknolojia za kidijitali kuleta usawa kwa ajili ya kuboresha maisha ya watu. Uzinduzi wa Vodacom Digital Skills Hub ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuwa vinara katika njia ya kuunda Afrika ya kidijitali na yenye usawa," alisema Shameel Joosub, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Group.

Vodacom Digital Skills Hub itatoa mafunzo ya ujuzi wa kidijitali yaliyothibitishwa na mamlaka husika huku mtu akijifunza kwa kasi yake binafsi kwa vijana kati ya umri wa miaka 18 na 35. Hii ni pamoja na majukwaa ya e-learning yaliyopo tayari katika masoko ya Vodacom kwenye nchi husika. 

Madarasa ya mtandaoni na e-learning yamewezesha wanafunzi katika maeneo ya mbali au yasiyohudumiwa kufikia elimu bora kupitia majukwaa kama Talimy nchini Misri, e-Fahamu nchini Tanzania, VodaEduc nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Faz Crescer nchini Msumbiji na jukwaa la e-learning nchini Afrika Kusini, likitoa rasilimali nyingi mtandaoni zinazokidhi mahitaji mbalimbali ya kujifunzia.

"Kama kampuni inayozingatia dhamira ya kuunganisha vijana kwa ajili ya mustakabali bora, tunafurahia mpango huu unaolenga kuhamasisha kizazi kipya cha wabunifu wa kidijitali. Lengo letu kuu katika mpango huu sio tu kusaidia upungufu wa ujuzi wa kidijitali barani Afrika bali pia kukuza vipaji vya vijana na hivyo kuendeleza mustakabali wa kidijitali wa Afrika, hivyo kuongeza fursa za uwezeshaji katika uchumi wa jumuishi wa kidijitali," alisema Vivienne Penessis, Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Vodacom Tanzania Plc.

Vodacom Digital Skills Hub imeanzishwa ili kuwawezesha vijana, hasa wasichana, kufikiria kazi katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati (STEM), na inajumuisha mafunzo ya vitendo ya ujuzi wa kidijitali kwa vijana barani Afrika. AWS Educate ni mojawapo ya programu za kwanza zitakazotolewa kupitia Vodacom Digital Skills Hub na kuongeza programu nyingine kwa majukwaa ya u-learning yaliyo katika nchi mbalimbali, zikiwa na lengo la kuwawezesha vijana katika maeneo ya STEM. Nchini Tanzania, AWS inakuja kama nyongeza kwa juhudi za kuhamasisha vijana wa Tanzania kama vile VYB, ambayo inalenga vijana wenye umri kati ya miaka 15 hadi 28.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: