Na Oscar Assenga, MKINGA.

MKUU wa wilaya ya Mkinga Mkoani Tanga Gilbert Kalima amezindua utoaji wa huduma ya Ufundi Umeme wa Majumbani kwenye Kaya 50 za wilaya hiyo mpango ambao unafanya na Chuo cha Veta ikiwa ni sehemu ya kutoa kazi zao kuwanufaisha wananchi ambao wanakabiliwa na changamoto hiyo kwenye maeneo yao.

Akizungumza mara baada ya kuzindua mpango huo,DC Kalima alisema kwamba kazi hiyo nzuri ambayo inafanywa na mafundi wa chuo hicho vijana inaonyesha umuhimu wao ndani ya wilaya hiyo kwa maana wanazaisha wataalamu ambao baadae wanakuja kuwa chachu ya maendeleo kwenye eneo hilo.

Alisema kutokana na mpango huo mzuri ambao wameuanzisha wanapaswa kupongezwa kwa uamuzi huo wa kuandaa na kuwasaidia wananchi 50 wenye changamto ya kuunganisha umeme kwenye nyumba zao katika wilaya ya Mkinga na hivyo kuchochea ukuaji wa maendeleo .
“Inawezekana ikafika mahali kuonekana hili ni jambo la kawaida lakini niwaambie kwamba wapo watu maeneo mengine wanatamani kupata huduma kama hii lakini hawawezi kuipata kutokana na kutokuwa na fursa ya kuwa na chuo kama hiki na kuwa na mitaala ambayo inaweza kuwaandaa watoto na kuwafanya kuwa mafunzo”Alisema
Aidha alisema jambo hilo ambalo limefanywa na veta ni kubwa huku akitaka liwe mfano kwa Taasisi nyengine ambazo zinatoa huduma kwenye wilaya ya Mkinga inayoendelea kukua tokea ilipoanzishwa mwaka 2006 na hivyo mpango huo utakuwa chachu ya maendeleo kwa jamii.

Awali akizungumza Mkuu wa Chuo cha Veta wilaya ya Mkinga alisema lengo la zoezi hilo ni kusaidia kupunguza gharama za kupata huduma ya umeme kwa kaya zenye zenye kipato cha chini katika tarafa mbili za wilaya ya Mkinga ambapo wameamua kuchangia gharama za Tanesco kwa kaya 50.
Alisema kukamilika kwa zoezi hilo kutazisaidia kaya zitakazonufaika kukuza uchumi wake katika shughuli zao za kujipatia kipato na pia kuimarisha ulinzi katika kaya hizo kwa kuwa na mwanga wa kutosha wakati wa usiku.
"Hivyo kwa kuanza kutekeleza zoezi hilo kwa kaya 50 chuo hicho kimeanza kumuingizia umeme Bibi Maria John Steven ambapo gharama zote zimegharamiwa na chuo cha ufundi Veta Mkinga na zoezi la kuashwa kwa Umeme litazunduliwa DC Mkinga”alisema .
Hata hivyo alisema kwamba gharama za vifaa kwa ajili ya kuingiza umeme kwenye kaya kwa wananchi wa kipato cha chini ni kubwa hivyo wanawaomba wadau ikiwemo Serikali ,Taasisi na Mashirika na watu binafsi kusaidia kuchangia mahitaji ya vifaa vya umeme ili kuwasaidia wananchi kupata huduma ya umeme ikiwa pia ni utekelezaji wa ilani ya CCM.

“Chuo chetu kina uwezo wa kufanya kazi za ufundi umeme majumbani ,utengenezaji wa thamani kama madawati ,vitanda vya chuma hivyo basi tunaomba kushirikishwa katika shughuli zinazoendelea na tunazozitoa katika chuo chetu ili tuongeze kipato na kuboresha mafunzo kwa wanachuo wetu”
Alisema Mkuu huyo wa Chuo.

Naye kwa upande wake Mkazi wa Kaya iliyowekewa Umeme Bibi Maria John Steven alimshukuru Rais kwa uwepo wa chuo cha Veta hapa Tanga kimetusaidia kupata umeme ambao ulikuea ni ndoto kwao.

Alisema kwamba wakati wanatumia vibatari kuwasha taa vilivyokuwa vanalipuka mara kwa mara na hivyo kuhatarisha usalama wao na jamii yao hivyo mpango huo utawasaidia pia kuweza kuwakwamua kiuchumi.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: