Na Burhani Yakub, Korogwe.
Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela ameombwa kuingilia kati mgogoro wa mirathi ya mwanamke mkongwe, Kabula Seni aliyefariki na kuacha nyumba iliyopo mtaa wa Msalala Road miti mirefu mjini Geita.
Mgogoro huo unadaiwa kuibuliwa na Diwani wa viti maalumu Geita, Khadija Mfuruki anayedaiwa kushinikiza fedha zitokanazo na mauzo ya nyumba hiyo zigawanywe kinyume na makubaliano ya vikao vya familia.
Ombi hilo limetolewa na Lulu Msemakweli ambaye ni msimamizi wa mirathi hiyo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Korogwe.
Amesema ameamua kumuomba Mkuu wa mkoa wa Geita kuingilia kati mgogoro huo kwa sababu Diwani huyo amekuwa akitumia madaraka yake kuvuruga mchakato wa mirathi.
Amesema chanzo cha mgogoro huo ni baada ya familia kuamua kuiuza nyumba na kupatikana mnunuzi ambaye aliweza kutoa malipo ya awali ya nyumba hiyo ndipo alipojitokeza na kulazimisha fedha zitumike kuwanunulia nyumba nyingine wajukuu wawili licha ya kuwa marehemu aliacha wajukuu 30.
"Amefikia hatua ya kumuamuru mteja anayenunua nyumba hiyo ya urthi asilipe awamu iliyobaki mnunuzi ameingia woga sana,tusichokubaliana naye ni kitendo cha kuamuru wajukuu wawili tu wajengewe nyumba na hawa wengine 28 watajisikiaje?", amesema Lulu.
Lulu ambaye amesema ni miongoni mwa watoto watatu walioachwa na mama yao wakiwamo wanaume wawili amesema kupitia mahakama alipitishwa kuwa msimamizi wa mirathi na kwamba anachohitaji ni maamuzi ya mgawanyo wa mirathi yafanywe na wanafamilia na siyo kutoka nje.
"Diwani amevuruga mno mchakato wa mirathi yetu ningeomba Mkuu wa mkoa aingilie kati ili muafaka upatikane.... natarajia kwenda ofisini kwake kumpa ombi letu hili", amesema Lulu.
Akizungumza kwa njia ya simu, Diwani Mfuruki amwsema siyo kweli kwamba ameingilia kati mirathi ya familia hiyo lakini kwa sababu yeye ni kiongozi hana budi kurekebisha pale anapolalamikia kuhusu haki ya wananchi katika eneo lake.
"Sijaingilia kati mirathi ifahamike kuwa mimi ndo niliyesaidia hata mchakato wa kesi mahakamani hadi wakashinda,yapo mengi ambayo si ustaarabu kuweka hadharani,ninachotaka ni kuhakikisha usawa pande zote... kila upande upate haki"amesema Diwani huyo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: