Na Mwandishi Wetu, WHMTH, Arusha.

Serikali inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu manufaa ya mfumo wa anwani za makazi hatua ambayo pamoja na masuala mengine itapunguza uharibifu wa miundombinu ya mfumo huo muhimu unaolenga kusaidia wananchi kuingia kwenye uchumi wa kidigitali.

Miongoni mwa masuala yaliyobainika katika zoezi linaloendelea la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi katika Halmashauri sita za Mkoa wa Arusha ni baadhi ya wananchi kutokuwa na uelewa wa kutosha kuhusu manufaa ya Mfumo wa Anwani za Makazi hali inayoathiri utunzaji wa miundombinu yake.
Hayo yamebainishwa tarehe 23 Agosti, 2024 Jijini Arusha na Mratibu wa utekelezaji wa Mfumo wa Anwani za Makazi wa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Jampyon Mbugi wakati akitoa ufafanuzi wa suala hilo lililobainika wakati wa zoezi la Uhakiki na usasishaji mkoani humo.

“Katika baadhi ya maeneo imeshuhudiwa uhalibifu wa aina tofauti wa miundombinu hiyo ambapo baadhi ya miundombinu imegongwa na magari na baadhi imekatwa. Aidha, maeneo mengine mbawa zinazoonesha majina ya barabara ama mitaa zimeng’olewa, zimefutwa ama kukunjwa”, amesema Mhandisi Mbugi.
Amesema zipo Sheria na Kanuni zinazosimamia utunzaji wa Miundombinu nchini ikiwa ni pamoja na Miundombinu hiyo ya Mfumo wa Anwani za Makazi na kwamba katika maeneo yote kwenye tatizo hilo Sheria za kutunza miundombinu zitachukua mkondo wake kwa wataokapatikana na kosa la kuharibu miundombinu.

“Serikali badala ya kujikita kwenye matumizi ya Sheria na Kanuni husika, imeanza na inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu manufaa ya Mfumo na umuhimu wa kutunza na kuendeleza miundombinu ya Mfumo. Elimu kwa umma itapunguza kwa kiasi kikubwa uharibifu wa miundombinu. Sambamba na hilo, tumeshuhudia kwa jinsi tunavyoendelea kutoa elimu uharibifu umeanza na unaendelea kupungua”, amesisitiza Mhandisi Mbugi na kuongeza.

“Mfumo ni nyenzo muhimu katika maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi ikiwa ni pamoja na uchumi wa kidijitali hivyo niwaombe wananchi wa Mkoa wa Arusha kusaidia kufanikisha zoezi la uhakiki kwa kutoa ushirikiano kwa wataalamu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa zote zinazohitajika” amesisitiza.

Wakati wa Ufunguzi wa Zoezi la Uhakiki wa Taarifa za Anwani za Makazi lililofanyika Kimkoa, mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala Msaidizi Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Mkoa wa Arusha Bw. David Lyamong, alitoa wito kwa Wananchi kutoa taarifa kuhusu uharibifu wa miundombinu hiyo mara tu wanapobaini Pamoja na kuhimizana kuilinda kwa mfumo wa ulinzi shirikishi kwani miundombinu hiyo imetengenezwa kwa gharama kubwa.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: