Viongozi wa Kampuni ya Qwihaya General Enterprises LTD inayojihusisha na biashara ya mbao wakikabidhi msaada wa mbao 2200 kwa kaya 50 za mitaa ya Buganda na Ilemela Mahakamani katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ambazo nyumba zao zilibomolewa na mvua Septemba 6 mwaka huu.

Na Mwandishi Wetu, Mwanza

KAMPUNI ya Qwihaya General Enterprises LTD inayojihusisha na biashara ya mbao imetoa msaada wa mbao 2200 kwa kaya 50 za mitaa ya Buganda na Ilemela Mahakamani katika Manispaa ya Ilemela mkoani Mwanza ambazo nyumba zao zilibomolewa na mvua Septemba 6 mwaka huu.

Kaya hizo zenye jumla ya wakazi 350 zimepewa msaada huo wa mbao kwa ajili ya kupaulia upya nyumba zao.

Msaada huo wenye thamani ya zaidi ya Sh.milioni 13.2 umekabidhiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni hiyo, Benedicto Mahenda Qwihaya kwa wakazi hao ikiwa ni kuitikia wito wa Serikali kwa wadau kujitokeza kusaidia waathirika wa janga hilo.

Kupitia msaada huo, kaya 16 za Mtaa wa Buganda ambao nyumba zao zilibomoka kabisa zimepata vipande 47 vya mbao huku kaya nyingine 13 ambazo nyumba zao hazikupata madhara makubwa zikipewa mbao 30 kila moja.

Msaada kama huo pia umetolewa kwa Kaya 21 kutoka Mtaa wa Ilemela Mahakamani ambao pia waliathiriwa na mvua hizo zilizowaacha wananchi wakilala nje kwa kukosa makazi.

Akikabidhi msaada huo, Mkurugenzi wa Qwihaya, Benedicto Mahenda amesema uongozi wa kampuni hiyo inayojihusisha na biashara ya mazao ya misitu uliguswa na taarifa za janga hilo zilizotangazwa kupitia vyombo vya habari ikiwaonyesha watoto, wazee na wanawake wakiwa wamelala nje kwa kukosa makazi baada ya nyumba zao kubomolewa.

“Tumetoa sehemu kidogo ya tulichojaaliwa na Mwenyezi Mungu kusaidia waathirika kujenga upya makazi yao,’’ amesema Mahenda.

Akishukuru kwa niaba ya wenzake, Regina Chrisant, mmoja wa waathirika, mkazi wa Mtaa wa Buganda ameishukuru kampuni ya Qwihaya, Serikali na wadau wote kwa misaada inayowawezesha kurejea katika maisha yao ya kawaida baada ya janga lililowaacha wakiwa hawana makazi.

‘’Misaada hii ya hali na mali imeturejeshea matumaini siyo kwa kwa kutuwezesha kuyajenga upya makazi yetu, bali pia inaonyesha jinsi Watanzania tunavyoishi kwa upendo miongoni mwetu,’’ amesema Regina.

Stanslaus Francis, mwathirika mwingine aliyepokea msaada ameomba wadau zaidi kujitokeza kusaidia waathirika kurejea katika maisha yao ya kawaida baada ya janga hilo ambalo alikusababisha majeruhi wala vifo.

Shukrani zingine zimetolewa na Diwani wa Kata za Shibula iliko Mtaa wa Buganda, Swila Dede (CCM) huku akiwaomba wadau wengine kujitokeza kuitikia wito wa Serikali wa kusaidia wananchi kwa sababu bado kuna mahitaji mengi ikiwemo ya chakula, samani za ndani na vifaa vingine vya ujenzi.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Buganda, Evarsit Chikanga amewataka wanaopokea msaada kuitumia kwa malengo mahusui ikiwemo kujenga upya makazi yao huku Mratibu wa Maafa Manispaa ya Ilemela, Jamses Wembe akiwataka wananchi wanaoishi jirani na fukwe na wanaofanya shughuli za kiuchumi na kijamii ndani ya Ziwa Victoria kuchukua tahadhari mvua na upepo mkali.

Kwa mujibu wa Wembe, tahadhari hiyo inatokana na utabiri iliyotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa (TMA) kuhusu uwezekano wa ukanda wa Ziwa Victoria kupata mvua nyingi utakaoambatana na upepo mkali ndani ya siku tano zijazo.
Viongozi wa Kampuni hiyo wakizungumza na waathirika wa nyumba hizo.
Waathirika wa nyumba hizo wakipokea msaada.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: