Dar es Salaam. Tarehe 31 Agosti 2023: Serikali imeipongeza Benki ya CRDB kwa hatifungani yake ya kijani yenye thamani ya dola za Marekani milioni 300 zitakazowekezwa kwenye miradi yenye mrengo wa kulinda mzingira.
Pongezi hizo zimetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais; Mipango na Uwekezaji, Mheshimiwa Kitila Mkumbo alipozindua uuzaji wa hatifungani hiyo jijini hapa. Profesa Kitila amewahimiza Watanzania kuanzia mtu binafsi, kampuni, taasisi za kimataifa hata mashirika ya umma.
“Hatifungani hii ni ya kihistoria sio tu katika sekta ya fedha nchini bali nchi za Kusini mwa Jangwa la Sahara kwani Benki ya CRDB inakuwa ya kwanza kuitoa. Ni hatifungani itakayowezesha kupata fedha za kutekeleza miradi ya kuhifadhi mazingira na yenye matokeo chanya kwa jamii yaani green, social and sustainability bond. Hatifungani hii pia ni ya kwanza kwa ukubwa Kusini mwa Jangwa la Sahara. Hongereni sana Benki ya CRDB,” amesema Profesa Mkumbo.
Waziri Mkumbo amesema kuuzwa kwa hatifungani hiyo, sio tu ni mafanikio kwa Benki ya CRDB inayoingia kwenye historiaya kutoa hatifungani yenyethamani kubwa zaidi Afrika kusini mwa Jangwa la Sahara bali Tanzania kwa ujumla.
“Mkifanikiwa kuuza hatifungani hii na mimi nitakuwa nimefanikiwa kwani nikienda kwa mheshimiwa Rais kumpa ripoti ya uwekezaji sitaacha kusema kuhusu hatifungani hii. Riba mnayotoa ya asilimia 10.25 ni kubwa na itawafaa wote watakaoinunua. Kama ambavyo sisi tunaenda kujifunza kwa wenzetu kuhusu masuala tofauti yatakayotufaa, nao waje kujifunza kuhusu hatifungani ya kijani,” amepongeza Waziri Mkumbo.
Uuzaji wa hatifungani hii, Waziri amesema ni hatua muhimu katika ustawi na maendeleo ya uchumi nchini kwani utachangia utekelezaji wa Mpango wa Taifa wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha yaani National Financial Sector Development Master Plan 2020/21 – 2029/30 wenye lengo la kuwezesha upatikanaji wa rasilimali fedha kwa ajili ya miradi katika sekta ya umma na binafsi ili kujenga uchumi shindani kwa maendeleo ya watu.
Akiongea na mamia ya wawekezaji, waandishi wa habari na wageni waalikwa waliojitokeza kwenye hafla ya uzinduzi wa uuzaji wa hatifungani hiyo utakaodumu mpaka Oktoba 6, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema uamuzi wa kutoa hatifungani hiyo umetokana na mahitaji makubwa ya mikopo pamoja na mwelekeo wa dunia katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
“Athari za mabadiliko ya tabianchi zimezigusa jamii nyingi duniani hivyo kulazimu kuunganisha nguvu za kukabiliana nazo. Mafuriko, ukame na mlipuko wa magonjwa ni baadhi ya matokeo ya mabadiliko haya ya hali ya hewa ambayo hatifungani ya kijani inakusudia kuwezesha miradi ya kukabiliana nayo. Nchi nyingi duniani zinatoa hatifungani hizi na sasa ni zamu yetu hivyo namwomba kila Mtanzania kujitokeza kuwekeza ili kwa pamoja tuyalinde mazingira yetu,” amesema Nsekela.
Licha ya jitihada mbalimbali zinazofanywa na wadau mbalimbali wa sekta ya fedha nchini ikiwemo Benki ya CRDB katika uwezeshaji wa miradi inayojali mazingira, bado jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi zinaendelea na mahitaji ya uwezeshaji wa miradi yenye mrengo huo ni makubwa kwani miradi mipya inabuniwa kila siku kuendana na kasi ya ukuaji wa teknolojia.
Hatifungani hii ya miaka mitano itauzwa kwa awamu lakini kwa awamu ya kwanza Benki ya CRDB inakusudia kukusanya mpaka shilingi 55 bilioni.
Akimshukuru Waziri kwa kutenga muda wake na kushiriki hafla hiyo, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Benki ya CRDB, Dkt Ally Laay amesema Afrika ni bara linaloathiriwa zaidi na mabadiliko ya tabianchi ingawa lenyewe linachangia kwa kiasi kidogo sana uchafuzi na uharibifu wa mazingira.
“Imekuwa kawaida hivi sasa kusikia majanga mfano mafuriko na kimbunga kama Freddy kilichotokea Malawi na Msumbiji, na Idai kiue Zambia au ukame na nzige walioharibu mashamba nchini. Majanga haya yote yanahitaji fedha nyingi kukabiliana nayo. Wakati wote, Benki ya CRDB imekuwa mfano wa kuleta bidhaa bunifu sokoni zinazosaidia kutatua changamoto za wateja wake na jamii nzima kwa ujumla. Kwa hatifungani hii, inaendelea kuonyesha mfano,” amesema Dkt Laay.
Mwenyekiti huyo ameishukuru Serikali na mamlaka zake zilizotoa ushirikiano mkubwa kufanikisha kutolewa kwa hatifungani hiyo itakayoorodheshwa katika Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) na Soko la Hisa London (LSE) la nchini Uingereza.
Uuzaji wa hatifungani hiyo unafanyika baada ya kukamilisha mchakato wa kisheria na kikanuni uliochukua zaidi yam waka mmoja ambao unaosimamiwa na Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA).
Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Nicodemus Mkama naye ameipongeza Benki ya CRDB kwa kufanikiwa kuitoa na kuiuza hatifungani hiyo inayokidhi vigezo vya kimataifa vya hatifungani za kijani.
“Ni matumaini yangu kwamba miradi mingi ya kimazingira itanufaika na fedha zitakazotokana na mauzo ya hatifungani hii. Nitumie fursa hii kuzihamasisha taasisi nyingine za fedha, mashirika ya umma na kampuni binafsi kutoa hatifungani zitakazosaidia kufanikisha maendeleo ya taifa letu,” amesema Mkama.
Katika safari ya kutoa hatifungani hiyo, Benki ya CRDB imeshauriwa kwa kiasi kikubwa na kampuni ya FSD Africa. Mkurugenzi wa Masoko ya Mitaji wa FSD Africa, Evans Osano amesema “kuuzwa kwa hatifungani hii ua kijani kunadhihirisha kukua kwa uchumi wa Tanzania na kudhihirisha fursa zilizopo kwa wawekezaji wa ndani hata wa kimataifa. Ikiwa ni hatifungani ya kwanza ya kijani kuuzwa Tanzania, inaongeza mjadala wa ajenda ya umuhimu wa uwekezaji endelevu barani Afrika. Tunayo furaha kuwa sehemu ya hatifungani hii kwa kutoa ushauri elekezi.”
Wengine waliofanikisha kutolewa kwa hatifungani hiyo ni Benki ya Stanbic ambayo ilikuwa mshauri mkuu wa upangiliaji huku Denton Tanzania Law Chamber ikitoa ushauri katika masuala yote ya kisheria. Orbit Securities Tanzania ndiye dalali mkuu wa hatifungani hiyo na kampuni ya KPMG ikitoa ushauri wa kihasibu. Kampuni ya Sustainalytics imesaidia kutoa maoni huru kwenye mchakato huo.
Ili kuwekeza kwenye hatifungani hii, mteja anatakiwa kutembelea tawi lolote la Benki ya CRDB au kwenda ofisi za wakala ambako atajaza fomu ambazo zinapatikana kwenye tovuti ya benki ambayo ni www.crdbbank.co.tz. Kwa ufafanuzi Zaidi anaweza kupiga simu idara ya huduma kwa wateja kwa kubofya namba 0800008000 bila makato yoyote.
Benki ya CRDB imekuwa kinara wa kutoa mikopo inaypolinda mazingira juhudi ambazo zilitambuliwa na Mfuko wa Mazingira Duniani yaani Green Climate Fund (GCF) hivyo kuwa taasisi ya kwanza ya fedha kusini mwa Jangwa la Sahara kukidhi vigezo vya mfuko huo.
Toa Maoni Yako:
0 comments: