Dar es Salaam. Tarehe 12 Juni 2023: Benki ya CRDB imeianza safari ya wiki mbili ya kuwapika wabunifu 196 waliochaguliwa kwenye programu yake ya Imbeju inayolenga kutoa mtaji wezeshi kwa vijana na wanawake.

Washiriki hao ni kati ya wabunifu 709 waliotuma maombi yao kuanzia Machi 12 program hiyo ilipozinduliwa na Waziri Mkuu Mh. Kassim Majaliwa Majaliwa (MB) na kukidhi vigezo vya awali vilivyowekwa.
Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amewapongeza washiriki waliofanikiwa kufika hatua hii akiwasisitiza kuwa ubunifu wao wa kipekee, shauku yao isiyoyumba, na jitihada zao katika ujasiriamali zimewaweka mbele ya kundi kubwa la washiriki waliowasilisha maombi yao hivyo kuwa sehemu ya fursa hii.

“Tunapoianza kambi hii ya mafunzo, ni wakati muhimu katika safari yenu ya ujasiriamali kwani mtapata fursa ya kuboresha bidhaa na huduma zenu, mikakati na kupata ujuzi muhimu unaohitajika ili kuwawezesha kufanikiwa katika hatua hii ya mwanzo katika uendeshaji wa biashara.

Niwasihi kujifunza kwa umakini mkubwa ili kutumia mafunzo na uzoefu mtakaoupata kuboresha biashara zenu. Kumbukeni kuwa maarifa ni nguvu na kwa kujijengea ufahamu na ujuzi sahihi, mtakuwa tayari kukabiliana na changamoto na kuchukua fursa nyingi zilizopo mbele yenu. Na hapo ndipo mafanikio ya programu hii yatakapoonekana,” amesema Nsekela.
Mkurugenzi huyo pia alisisitiza dhamira isiyoyumba ya Benki ya CRDB kusaidia kukuza biashara changa nchini kupitia mitaji wezeshi hasa zile zinazomilikiwa na vijana na wanawake, makundi muhimu yasiyopewa kipaumbele kwenye fursa za uchumi.

Nsekela amesisitiza kuwa Benki ya CRDB inaelewa kuwa upatikanaji wa fedha ni jambo muhimu katika kubadilisha mawazo bunifu kuwa biashara endelevu hivyo programu ya IMBEJU inalenga kuchochea mafanikio ya wabunifu na waanzilishi wa biashara na kuhakikisha fedha haiwi kikwazo cha safari yao ya ujasiriamali.

“Benki ipo tayari kuwekeza katika ndoto zenu na kutoa rasilimali muhimu za kusaidia biashara na mawazo yenu kukua na kufikia mafanikio makubwa zaidi.

Tunaamini sehemu kubwa ya kushindwa kwa biashara nyingi changa ni kukosa ujuzi wa usimamizi, kutotambua vihatarishi vya biashara na kutotambua fursa za ukuaji. Unaweza kuwa na fedha na mtaji lakini usipokuwa na uelewa na ujuzi sahihi huwezi kufanikiwa, hii ndio sababu iliyotufanya kuwekeza katika mafunzo yenu. Ujasiriamali ni njia iliyojaa vikwazo lakini msikate tamaa. Mnatakiwa kujua katika safari yenu mtakabiliana na vikwazo vingi, na kupitia nyakati zenye changamoto na haya mafunzo haya ni sehemu ya nyenzo muhimu ya kupambana na changamoto hizi,” amesisitiza Nsekela.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amesema wanatambua kuwa mtaji si kikwazo pekee cha vijana wenye mawazo bunifu kuyageuza kuwa biashara inayotatua changamoto za jamii kwani takwimu zinaonesha biashara nyingi changa zimekufa si kwa sababu ya mtaji bali kutokana na kukosa maarifa sahihi ya usimamizi na uendeshaji wa biashara.

“Leo tupo hapa kutekeleza kile tulichoahidi kwa maana ya kutoa mafunzo yanayolenga kuwaongezea uwezo vijana walioomba mtaji wezeshi wa Imbeju ili ikifika hatua ya kuwawezesha kwa mtaji, wawe tayari kutumia mtaji huo kwa ufanisi na kuleta matunda yaliyokusudiwa.

Pia tunatambua si wote wataweza kufika hatua ya kupata mtaji wezeshi, hivyo basi elimu itakayopatikana hapa bado itakuwa sehemu ya uwezeshaji wa maarifa ambao ni mchango katika kukuza bunifu zenu,” amesema Tully.
Tully aliwaeleza pia kuwa zimetengwa fedha kiasi cha TZS 5 bilioni kwa ajili ya kuwawezesha vijana wenye miradi ya ubunifu pamoja na wanawake hivyo wawe makini na washiriki kambi kikamilifu kwa sababu kambi hii ni sehemu ya mchujo kabla ya kupewa mtaji wezeshi.

Programu ya Imbeju inatekelezwa katika madirisha mawili, la kwanza ni la ushindani linaloshindanisha miradi ya ubunifu itakayopewa mtaji wezeshi ambalo linaendeshwa kwa ushirikiano na Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na Tume ya TEHAMA (ICTC) ikiwalenga vijana na wanawake. Dirisha la pili ni mahsusi kwa wanawake hasa waliopo kwenye vikundi. Tangu kuzinduliwa kwa programu ya Imbeju mpaka Mei 31, dirisha hili limetoa mafunzo kwa vikundi vya wanawake 1,341 vyenye wanachama 18,614 nchini.
Vijana wengi, Mkurugenzi Mkuu wa COSTECH, Dkt Amos Nungu amesema wanaamini mtaji ni fedha tu bila kufahamu kuwa hata wazo pekee ni mtaji ambalo mwenye nalo akishikwa mkono anaweza kulifanya biashara kwa kutatua kero iliyopo katika jamii.

Wanachokifanya COSTECH, amesema ni kuboresha wazo la mbunifu yeyote nchini na kwa kushirikiana na Benki ya CRDB kumpa mkopo wezeshi wa kulitekeleza.

"Muhimu ni uhakika wa kurudisha fedha ambazo mbunifu atapatiwa. Mafunzo haya yanaangalia uwezo wa mbunifu kuisimamia biashara yake kwa kujiridhisha kama anazo rasilimali za msangi mfano watu wa kutosha kumsaidia katika uendeshaji, kuangalia kama ni wakati sahihi wa kuiingiza bidhaa au huduma yake sokoni na kumjenga kwa elimu ya usimamizi na uendeshaji biashara pamoja na elimu ya fedha," amesema Dkt Nungu.
Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya TEHAMA (ICTC), Dkt. Nkundwe Mwasaga amesema ICTC ina kazi kuu mbili, kwanza ni kuratibu kazi na shughuli za TEHAMA nchini na kutekeleza sera ya Taifa ya TEHAMA.

Kinachofanywa katika kambi hii ya Benki ya CRDB, amesema ni kuwajenga ili waweze kukuza biashara zenu na wakati wanakua wawe na ufahamu juu ya matarajio ya taasisi mbalimbali wezeshi kama Benki ikiwa ni pamoja na maswali yanayoulizwa kwa wajasiriamali wabunifu na benki pale uwezeshaji wa benki unapohitajika.

"CRDB ni benki kubwa nchini na kikanda. Nyote mliopo hapa mmepata nafasi nzuri ya kuziongezea sifa biashara zenu. Ni hatua nzuri mnayopaswa kujivunia," amesema Dkt Nkundwe.


Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: