Viongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mtaa wa Mwembeni wilayani Manyoni na Viongozi wa Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) wilayani humo wakiwa kwenye kikao cha kupanga mikakati ya kutokomeza ukatili wa kijinsia kilichofanyika jana May 29, 2023.

Na Dotto Mwaibale, Manyoni.

KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tawi la Mwembeni Wilaya ya Manyoni mkoani Singida kwa kushirikiana na Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA wamekutana katika kikao kazi cha kuweka mikakati kabambe ya kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wilayani humo.

Akizungumza na waandishi wa habari Katibu wa SMAUJATA Wilaya ya Manyoni Shujaa Napegwa Jared alisema kikao hicho ni cha muhimu sana katika kutokomeza ukati katika wilaya hiyo hasa kitongoji cha Mwembeni.

"Tumekutana leo na wenzetu wa Kamati ya Siasa ya CCM wa kitongoji cha Mwembeni kwa lengo la kuweka mikakati ya pamoja ya kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia wilayani kwetu pamoja na eneo la Mwembeni ambalo lina watu wengi kutokana na kuwa ndani ya mji wa Manyoni na kuwepo kwa vitendo hivyo," alisema Jared.

Alisema CCM inanafasi kubwa katika kusimamia mmomonyoko wa maadili ya jamii ukiwemo ukatili wa kijinsia ndio maana wakaona ni vema wakae pamoja kwa lengo la kuongeza nguvu ya kukabiliana na jambo hilo ambalo limeonekana kukithiri maeneo mengi hapa nchini hususani katika wilaya hiyo.

Alisema wilaya ya Manyoni ni kongwe na inamwingiliano wa watu wengi kutoka sehemu mbalimbali jambo ambalo limechangia kuwepo na vitendo vya ukatili hasa kwa wanawake na watoto.

Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Kitongoji cha Mwembeni, Salutary Naaly, alisema kikao hicho cha pamoja SMAUJATA na Kamati ya Siasa ya CCM ya eneo hilo kitaleta tija kubwa katika mapambano ya kutokomeza ukatili wa aina yoyote ile kwenye wilaya hiyo na kitongoji hicho.

"Kitongoji chetu hiki kimekuwa na muingiliano wa watu wengi na kusababisha kuwepo kwa ukatili wa kijinsia, kupitia ushirikiano huu tutapiga hatua kubwa kukabiliana na vitendo hivyo kwani umoja ni nguvu," alisema Naaly.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Tawi la Mwembeni, Joseph Sajilo alisema kupitia umoja na ushirikiano huo hakuna jambo litakalo shindikana katika kukabiliana na kutokomeza vitendo hivyo wilayani humo hasa katika kitongoji hicho.

"CCM ni Chama kikubwa na ndicho kimekamata dola hivyo napenda kuwaambia kuwa kwa ushirikiano huu hatutashindwa kutokomeza ukatili katika wilaya yetu na hapa Mwembeni," alisema Sajilo.

Katika kikao hicho ajenda kubwa ilikuwa ili kutokomeza vitendo hivyo ni kudumisha ushirikiano, umoja na upendo baina ya wananchi, SMAUJATA, CCM na vyombo vya dola.
Kikao hicho kikiendelea.

Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: