Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Kimweri (mwenye kanzu) akimkabidhi mshindi wa kampeni ya Benki ni SimBanking, Mayani Yahaya Hassan mkazi wa Dodoma funguo ya gari baada ya kuibuka kidedea katika droo iliyochezwa mapema mwezi huu. Wengine pichani ni wafanyakazi wa Benki ya CRDB ambao walishiriki katika hafla hiyo ya kukabidhi gari kwa mshindi iliyofanyika siku ya Ijumaa tarehe 14 Aprili 2023. Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Kimweri (wapili kulia) na Meneja wa Benki ya CRDB Kanda ya Kati, Chabu Mishwaro (kulia) wakishuhudia mshindi wa kampeni ya Benki ni SimBanking, Mayani Yahaya Hassan mkazi wa Dodoma akikata utepe kama ishara ya kukabidhiwa gari baada ya kuibuka kidedea katika droo iliyochezwa mapema mwezi huu. Wengine pichani ni wafanyakazi wa Benki ya CRDB ambao walishiriki katika hafla hiyo ya kukabidhi gari kwa mshindi iliyofanyika siku ya Ijumaa tarehe 14 Aprili 2023.
---
Benki ya CRDB imekabidhi gari aina ya Toyota Crown kwa mshindi wa kampeni ya “Benki Ni SimBanking” kwa mwezi Februari na Machi anayejulikana kwa jina la Mayani Yahaya Hassan mkazi wa Dodoma.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi zawadi kwa mshindi huyo iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, Dodoma, Meneja wa Kanda ya Kati wa Benki ya CRDB, Chabu Mishwaro alisema mshindi huyo alipatikana katika droo ya kwanza ya kampeni hiyo iliyofanyika tarehe 6/04/2023.
“Mayani ni moja ya wateja ambao wamekuwa wakitumia SimBanking kufanya miamala yao ya kifedha, jambo ambalo lilimpelekea kuingia katika kinyang’anyiro cha ushindi, na kuibuka kidedea baada ya droo kuchezeshwa,” alisema Chabu.
Chabu alibainisha kuwa katika kusaidia jitihada za Serikali za kuchochea uchumi wa kidijitali nchini, kampeni ya “Benki Ni SimBanking” imekuwa ikihamasisha wateja kufanya miamala kidijitali kupitia SimBanking na kuachana na matumizi ya pesa taslimu.
Akielezea kampeni hiyo inaendeshwa, Chabu alisema kampeni ya “Benki Ni SimBanking” inaendeshwa kwa muda wa miezi 10 hadi Desemba 2023, ambapo kila siku wateja wamekuwa wakijishindia zawadi, huku pia kukiwa na zawadi za mwezi, miezi miwili, na zawadi kubwa ya Toyota Vanguard ambayo itatolewa mwishoni wa kampeni.
“Hadi kufikia sasa tayari tumeshatoa zawadi mbalimbali ikiwamo pesa taslimu, simu janja, na laptop kwa washindi 79. Zawadi bado zipo nyingi sana, hivyo niwasihi wateja na wale wasio wateja waendelee kufanya miamala kupitia SimBanking ili waweze kujishindia,” alisema chabu huku akiwakaribisha wale ambao sio wateja wa Benki ya CRDB kufungua akaunti ili waunganishwe na SimBanking.
Akikabidhi zawadi hiyo ya gari kwa mshindi, Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Kimweri aliipongeza Benki ya CRDB kwa kuandaa kampeni hiyo ambapo alisema sio tu inachochea matumizi ya mifumo ya kidijitali ya utoaji huduma, bali pia inachochea ujumuishi wa kifedha kwa wananchi.
Kimweri alisema Serikali imekuwa ikitilia mkazo katika matumizi ya TEHAMA katika utoaji wa huduma kwa wananchi ili kuendana na kasi ya maendeleo kote duniani, hivyo aliwasihi wateja na wananchi kutoa ushirikiano kwa Benki ya CRDB na kushiriki katika kampeni hiyo ya “Benki ni SimBanking”.
“Nimefurahi kuona Dodoma tumetoa mshindi katika kampeni hii, inaonyesha ni namna gani wananchi wa Dodoma wanaendelea kujenga uelewa juu ya umuhimu wa matumizi ya mifumo ya kidijitali ya kibenki. Niwasihi na wananchi wengi tujenge utamaduni wa kutumia mifumo hii si tu kwasababu ya zawadi bali tufanye hivyo tukitambua huko ndipo dunia ilipo sasa hivi,” aliongezea.
Akizungumza baada ya kutangazwa mshindi wa shindano hilo Mayani Yahaya Hassan aliishukuru Benki ya CRDB kwa zawadi hiyo ya gari huku akibainisha siri ya ushindi ni kujenga utamaduni wa kutumia SimBanking kufanya miamala yake yote ya kifedha.
“Ninafurahia sana kufanya miamala kupitia SimBanking iliyoboreshwa, imekuwa rahisi na nafuu sana kutumia. Sasa hivi miamala yangu yote nakamilisha kupitia SimBanking, iwe kufanya malipo kupitia CRDB Lipa Namba, kutuma pesa, kulipia bima, kulipia kodi na kutoa fedha kwa CRDB Wakala/ ATMs na Tawini bila ya kadi,” alibainisha Mayani.
Toa Maoni Yako:
0 comments: