Na Mwandishi wetu, Mirerani

UZINDUZI wa wiki ya usalama barabarani Wilayani Simanjiro umeanza kwa Mkuu wa kikosi cha usalama barabarani Mkoa wa Manyara (RTO) Georgina Richard Matagi kukamata basi bovu lililouwa limebeba abiria.

RTO Matagi amezindua wiki ya usalama barabarani mji mdogo wa Mirerani na kufanya ukaguzi wa magari mbalimbali na kutoa elimu kwa madereva wa pikipiki wanaobeba abiria (bodaboda).

Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, RTO Matagi amesema amelazimika kuzuia basi la kampuni ya Zacharia lililokuwa linatoka Orkesumet kwenda jijini Arusha kupitia Mirerani kutosafiri hadi lifanyiwe matengenezo kutokana na makosa mbalimbali lililokuwa nalo.

Matagi amesema basi hilo linaweza kusababisha ajali kwani matairi yake ni mabovu hayawezi kustahimili safari ndefu kwani yanaweza kupasuka wakati yakiendelea na safari.

“Pia tumebaini basi hilo linaweka mafuta kidogo ya sh10,000 kila baada ya kilomita kadhaa wakishachukua nauli za abiria badala ya vituo vya mafuta na kupatiwa risiti,” amesema RTO Matagi.

Amesema pia wamebaini ubovu wa breki za basi hilo, hivyo linahitajika kufanyiwa matengenezo kisha likaguliwe upya na ndiyo liweze kuendelea tena na safari ya kubeba abiria.

Amesema hata mfumo wa kuzima basi hilo umekuwa tofauti hivyo amewaagiza wahusika washushe abiria na walifanyie matengenezo ili waendelee na safari yao pindi likitengemaa.

Hata hivyo, dereva wa kampuni ya basi la Zacharia, John Aloyce amekiri mapungufu mbalimbali yaliyopo kwenye gari hilo lililokuwa likitoka kutoka Orkesumet hadi jijini Arusha.

Aloyce amesema amefikisha mapungufu yaliyopo kwenye basi hilo kwa mmiliki wake ila bado utekelezaji wake haukufanyika na kusababisha kukamatwa na kushindwa kuendelea na safari.

Amesema baadhi ya abiria ambao wanaendelea na safari yao imewabidi wahamie kwenye basi jingine la Simanjiro ili waweze kwenda jijini Arusha ila wale wa Mirerani wamefika.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: