Wakazi wa Moshi mkoani Kilimanjaro wameonekana kuipokea vyema promosheni ya “Benki ni SimBanking” ikiwa ni sehemu ya jitihada za Benki ya CRDB kuongeza ujumuishi wa Watanzania kwenye huduma za kibenki. Wakazi hao waliojitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa promosheni hiyo mkoani Moshi walionyesha kufurahia huduma zinazopatikana katika huduma ya SimBanking ambazo kwa kiasi kikubwa zimeondoa ulazima wa mteja kutembelea matawi ya benki iwe kufungua akaunti au kufanya miamala.
Akizungumza na mamia ya wateja waliojitokeza katika uzinduzi wa promosheni hiyo, Kaimu Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa Benki ya CRDB, Emmanuel Kafui ameeleza kuwa anatamani kuona huduma ya SimBanking inakua sehemu ya maisha ya kila siku ya wakazi wa Moshi wanapohitaji kufanya malipo, kutuma fedha pamoja na huduma nyingine za kifedha.
“Pamoja na kuwa na zawadi mbalimbali ambazo zitatolewa kwa watumiaji wazuri wa SimBanking katika kipindi cha promosheni ya Benki ni SimBanking, lengo letu kuu ni kufikisha huduma hii kwa kila Mtanzania jambo ambalo litakwenda kuongeza ujumuishi wa huduma za fedha na kuondoa utamaduni wa kufanya malipo kwa fedha taslimu” alisisitiza Kafui.
Takwimu za robo ya mwisho wa mwaka 2022 za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonyesha kuwa kuna watumiaji wa simu zaidi ya Milioni 58 huku watumiaji wa intaneti wakiwa zaidi ya Milioni 31. Ikiwa idadi hii yote itaweza kufikiwa na huduma za benki kwa njia ya simu basi Tanzania itakua imepiga hatua kubwa katika ujumuishaji wa huduma za benki kwa wananchi wake.
Kwa upande wake Meneja wa Tawi la Benki ya CRDB Moshi, Pamela Mushi amesema kuwa zawadi zenye thamani ya zaidi ya Shilingi Milioni 565 zitatolewa kwa wateja ambao watafungua akaunti kwa njia ta SimBanking na kufanya miamala mingi zaidi katika kipindi cha promosheni.
“Promosheni ya Benki ni SimBanking inakwenda kuwazawadia wateja wetu ambao ni watumiaji wazuri wa huduma ya SimBanking ambapo fedha taslimu zaidi ya Milioni 350, simu janja 200 sambamba na magari sita (Toyota Crown tano na Toyota Vanguard moja) yanakwenda kutolewa kwa wateja wetu" alisema Pamela.
Promosheni ya Benki ni SimBanking inakuja ikiwa ni kipindi kifupi kimepita baada ya Benki ya CRDB kutangaza taarifa ya fedha ya mwaka 2022 inayoonyesha kuongezeka kwa miamala ya kidigitali ambapo kwa mwaka 2022 zaidi ya asilimia 86% ya miamala ya wateja ilifanywa kwa njia za kidigitali hususan huduma ya SimBanking.
Meneja wa Tawi la Benki ya CRDB Moshi, Pamela Mushi akichukua alama za vidole katika zoezi la kuwafungulia wateja akaunti kupitia huduma ya SimBanking wakati wa promosheni ya kampeni ya 'Benki ni SimBanking' iliyofanyika leo Moshi, Kilimanjaro.
Toa Maoni Yako:
0 comments: