Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango ametoa wito kwa wamiliki wa kampuni na taasisi binafsi nchini kuhamasisha na kuzipatia uzoefu kampuni zinazochipukia (business startups) ili kuongeza wigo wa Sekta Binafsi ambazo zitakuwa chachu ya mageuzi makubwa ya baadae hapa nchini.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya sekta binafsi 2022 nchini Tanzania iliofanyika Masaki Jijini Dar es salaam.
Amesema Serikali imedhamiria kufanya kazi na Sekta Binafsi katika miradi mbalimbali ya ubia kama vile ujenzi wa barabara, miradi ya umwagiliaji na uzalishaji wa nishati hivyo ameiagiza Wizara ya Fedha na Mipango kwa kushirikiana na TPSF kukaa pamoja na kuangalia namna ya kuongeza ushiriki wa Sekta hiyo katika miradi ya ubia ili kukabiliana na mwitikio mdogo uliopo.
Pia Makamu wa Rais amesema bado Sekta Binafsi haifanyi vizuri katika kuchangamkia fursa mbalimbali na rasilimali za kimataifa katika kulinda mazingira.
Amewasisitiza wadau wote wa Sekta Binafsi chini ya TPSF kwa kushirikiana na Ofisi ya Makamu wa Rais - Mazingira, Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, na Ofisi za Ubalozi kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki kuchangamkia rasilimali fedha za kulinda mazingira kama vile biashara ya hewa ukaa na Green Climate Fund kuibua miradi ya utunzaji wa mazingira ikiwa pamoja na utengenezaji wa nishati mbadala, viwanda vya kuchakata taka ngumu na miradi mingine ya aina hiyo.
Aidha ameiagiza Wizara ya Viwanda na Biashara kuongeza kasi ya utekelezaji wa Mpango wa Maboresho ya Mazingira ya Biashara (National Blueprint) kwa kuhakikisha wanatekeleza shughuli zilizopangwa katika Mpango huo kufikia asilimia 50 mwezi Disemba 2023 kutoka kiwango cha sasa cha asilimia 13 na
kuzichukulia hatua taasisi ambazo hazitaki kubadilika na zinakwamisha
utekelezaji wa Blueprint.
Makamu wa Rais amesema Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji hapa nchini kwa lengo kuu la kuvutia uwekezaji, kukuza biashara na kukuza ushindani wa Sekta Binafsi. Amesema serikali imeendelea kupambana na kupunguza ukiritimba, urasimu na majukumu
kinzani katika Taasisi za Umma na kufuta utitiri wa kodi na tozo zisizo na tija.
Pia ametaja hatua zilizochukuliwa katika kuboresha uwekezaji ikiwemo Bunge kupitisha Sheria Mpya ya Uwekezaji ya Mwaka 2022 ambayo inatoa fursa
sawa kwa wawekezaji wote pamoja na kusainiwa kwa Mikataba ya Kutotoza Kodi Mara Mbili na nchi kumi (10) ili kuvutia na kuimarisha biashara na uwekezaji.
Kwa upande wake Waziri wa Viwanda na Uwekezaji Dkt. Ashatu Kijaji amesema serikali kupitia wizara hiyo imeendelea na jitihada za kuweka mazingira wezeshi ili kuweza kutumia vema eneo huru la biashara Barani Afrika kwa manufaa ya taifa ikiwemo sekta binafsi. Ametoa wito kwa sekta
binafsi kuweza kulifikia soko hilo kwa kupeleka bidhaa zinazoweza kununulika
na zenye uzalishaji endelevu.
Awali akitoa taarifa ya maendeleo ya Sekta Binafsi nchini , Mwenyekiti wa Sekta hiyo Bi. Angelina Ngalula ameishukuru serikali kwa mazingira bora na yenye haki ya ufayaji biashara nchini pamoja kudhibiti kwa kiasi kikubwa mfumuko wa bei,kuimarisha mahusiano ya sekta binafsi na ya Umma nchini, kuondolewa kwa vikwazo vya kibiashara katika masoko ya kikanda pamoja na kufunguliwa kwa masoko makubwa ya kimataifa.
Ameongeza kwamba sekta binafsi inamshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake binafsi za kuimarisha sekta ya utalii kupitia filamu ya Royal Tour mara baada ya changamoto za Uviko 19.
Pia amesema serikali imeimarisha sekta binafsi kwa kutoa ruzuku kwa wakulima na kupungua kwa riba za mikopo katika mabenki hapa nchini, kuwezesha mikopo kwa wanawake wafanyabiashara pamoja na wafanyabiashara wadogo wadogo kutengewa sehemu maalumu kwaajili ya biashara zao.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia viongozi na wadau wa Sekta Binafsi nchini wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2022yaliofanyika Masaki Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akisikiliza salamu mbalimbali za wadau wa Sekta Binafsi nchini wakati alipohudhuria Maadhimisho ya Siku ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2022 yaliofanyika Masaki Jijini Dar es salaam.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikabidhi tuzo ya mshindi wa kwanza wa kampuni yenye mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii ambaye ni Grumeti Reserve wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2022 yaliofanyika Masaki Jijini Dar es salaam.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa tuzo mbalimbali zilizotolewa wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Sekta Binafsi Tanzania kwa mwaka 2022 yaliofanyika Masaki Jijini Dar es salaam.
Toa Maoni Yako:
0 comments: