Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KATIBU wa Utikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Shaka Hamdu Shaka ametembelea kijiwe cha Kahawa Lumumba kilichopo Tabora Mjini na kunywa kahawa na wananchi waliokuwepo huku akitumia nafasi hiyo kuelezea hatua zinazochukuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika sekta ya kilimo.

Shaka amekuwa na utaratibu wa kukutana na wananchi wa maeneo mbalimbali anapokuwa kwenye ziara za kuangalia utekelezaji wa Ilani ya CCM na alipofika Mkoa wa Tabora alifika kwenye kijiwe hicho na kukutana na wananchi walikuwepo hapo.

Akiwa katika kijiwe hicho cha Kahawa Shaka pamoja na mambo mengine alitoa nafasi ya kusikiliza wananchi hao ambao walitoa pongezi kwa Rais Samia na Chama Cha Mapinduzi kwa kazi nzuri wanayofanya ya kuleta maendeleo na kusimamia utekelezaji wa Ilani.

Aidha wananchi hao walitoa ombi kwa Shaka kufikisha salamu zao kwa Rais Samia wakimuomba aendelee kuongeza fedha kwa ajili ya sekta ya kilimo ambayo watanzania wengi wanajihusisha nacho.Pia walitoa ombi la kupunguzwa kwa gharama ya maji ambayo wameeleza ni kubwa sana.

Baada ya maelezo hayo Shaka ameelezea hatua kwa hatua mipango inayoendelea kutekelezwa na Serikali inayoongozwa na Watanzania kuhakikisha maendeleo yanafika maeneo yote huku akieleza pia kuhusu juhudi za Rais katika kuboresha sekta ya kilimo.

“Rais Samia kwa kutambua umuhimu wa sekta ya kilimo ameendelea kuchukua hatua mbalimbali na miongoni mwa hatua hizo kuongeza fedha katika bajeti ya kilimo kutoka Sh.bilioni 254 mpaka Sh.bilioni 999.Ni ongezeko kubwa na ataendelea kuongeza kidogo kidogo hadi mambo yatakuwa sawa.”

Kuhusu changamoto ya bei kubwa ya ulipaji maji kwa wananchi wa Tabora Mjini, Shaka amesema atalifikisha suala hilo kwa Waziri wa Maji Jumma Aweso kuona hatua gani zinaweza kuchukuliwa kupunguza bei ya maji kama ambavyo wananchi wanaona.

Kwa upande wake Mbunge wa Tabora Mjini kwa tiketi ya CCM Emmanuel Mwakasa amesema ni kweli kuna changamoto kwenye eneo la bei ya maji ambayo imekuwa kubwa na wameshafikisha kilio cha wananchi kwa Waziri wa Maji lakini pia kwa Mamlaka ya Maji Tabora.

Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, (katikati) akizungumza na wananchi katika kijiwe cha kahawa Lumumba, mjini Tabora.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: