Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Antony J. Blinken alizindua Ripoti ya Mwaka 2022 ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mwaka huu, Tanzania ilionekana kukidhi vigezo vya kupandishwa hadi daraja la pili (Tier 2), ikimaanisha kwamba japokuwa bado Serikali ya Tanzania haijakidhi vigezo vyote vya kutokomeza usafirishaji haramu wa binadamu, lakini imefanya jitihada kubwa kuelekea azma hiyo.
“Marekani imepokea kwa furaha hatua kubwa iliyopigwa na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu ikilinganishwa na hali ilivyokuwa katika vipindi vilivyotolewa taarifa hapo awali,” alisema Balozi wa Marekani nchini Tanzania Donald Wright. “Ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam unaipongeza serikali ya Tanzania, Sekretarieti ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu, vyombo vya usimamizi wa sheria, idara ya ustawi wa jamii, taasisi katika sekta ya sheria, mashirika yasiyo ya kiserikali na wabia wengine kwa mafanikio yaliyofikiwa mwaka uliopita katika kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu.”
Ripoti ya Mwaka ya Usafirishaji Haramu wa Binadamu ni nyaraka ya kina kuhusu jitihada za serikali – ikiwemo serikali yetu – ikiangazia pia dhamira ya serikali ya Marekani ya kuongoza jitihada za kimataifa katika suala hili muhimu linalohusu haki za binadamu, utawala wa sheria na usalama wa taifa.
Ripoti ya mwaka 2022 imetaja hatua kadhaa zilizopigwa na serikali ya Tanzania ikiwemo kufanya uchunguzi wa kesi nyingi zaidi za usafirishaji haramu wa binadamu, kuwabaini waathiriwa wengi zaidi wa biashara hii, na kuwa na uratibu mzuri na taasisi za kitaifa na kimataifa ili kuimarisha mafunzo kwa maofisa wa serikali. Zaidi ya hayo, serikali ilipitisha Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu wa 2021-2024 (National Action Plan to Combat Trafficking in Persons) na kufanya marekebisho makubwa katika Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu ya Mwaka 2008. Nyingi ya jitihada hizi zilifanywa kwa ushirikiano na asasi za kiraia, ikiwemo Wanasheria Wasio na Mipaka (Lawyers Without Borders) na Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Dawa za Kulevya na Uhalifu (United Nations Office on Drugs and Crime) kupitia ufadhili wa Serikali ya Marekani. Ushirikiano kati ya serikali na asasi za kiraia ni muhimu sana katika utekelezaji wa shughuli za kujenga uelewa kwa lengo la kuzuia usafirishaji haramu na kuwasaidia waathiriwa wa biashara hii.
“Tunaihimiza Serikali ya Tanzania kupanua zaidi kazi nzuri iliyofanyika katika kipindi cha mwaka uliopita,” alisema Balozi Wright. “Tunatarajia kuongeza msaada wetu kwa Tanzania katika jitihada zake za kukabiliana na usafirishaji haramu wa binadamu Tanzania Bara na Zanzibar.”
Jitihada hizi zinaweza kujumuisha kuchukua hatua mahususi katika maeneo muhimu yafuatayo: kwa kuzingatia sheria na haki za binadamu, kuhakikisha kuwa wote wanaothibitika kuwa na hatia ya usafirishaji haramu wa binadamu wanahukumiwa vifungo virefu; kuongeza ulinzi kwa waathiriwa wanaotoa ushahidi katika michakato ya utekelezaji wa sheria; kupanua utoaji huduma kwa waathiriwa wa biashara hii kwa ushirikiano na mashirika yasiyo ya kiserikali; kutenga rasilimali fedha na watu kwa ajili ya Kamati na Sekretarieti ya Kukabiliana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu; na kupitisha na kutekeleza Sheria ya Kuzuia Usafirishaji Haramu wa Binadamu ya Mwaka 2008 visiwani Zanzibar.
Toa Maoni Yako:
0 comments: