Na John Walter-Manyara
Wafanyakazi wameiomba Serikali kupitia kwa Rais Samia Suluhu Hassan kuwaongezea Mishahara na maslahi Bora ili kumudu gharama za Maisha.
Wametoa kilio hicho leo Katika Sherehe za Mei Mosi mkoani Manyara zilizofanyika kimkoa katika uwanja wa Kwaraa mjini Babati.
Sherehe za Mei Mosi mwaka huu kitaifa zimefanyika jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri na kubebwa na kauli mbiu isemayo Mishahara na maslahi Bora ndo kilio chetu na kazi iendelee.
Kauli mbiu hiyo inaiimiza serikali kupandisha Mishahara na kuwaboreshea maslahi wafanyakazi kuendana na hali ya maisha ilivyo kwa sasa. Hata hivyo wamempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwapandisha madaraja watumishi katika sekta mbalimbali.
TUICO mkoa wa Manyara katika risala yao, wamesema changamoto zilizopo ni pamoja na Kutopandishwa vyeo kwa wakati,Kutopandishwa kwa Mishahara huku wakitaka kikokotoo Cha zamani kiendelee kufanya kazi.
Wamesema Kutoongezwa kwa Mishahara kwa watumishi kunasababisha mazingira magumu ya kazi hali inayopunguza morali katika kazi kwani wengine wamekuwa wakijaribu kujishughulisha na kazi zingine ili kumudu gharama za Maisha.
Risala hiyo iliyosomwa na Katibu wa Chama Cha Wafanyakazi wa Viwanda,Biashara, Taasisi za fedha,huduma na ushauri (TUICO) mkoa wa Manyara Juma Makanyaga, imesema kero nyingine iliopo ni baadhi ya waajiri kutoitisha mabaraza ya Wafanyakazi kama Sheria inavyotaka.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TUCTA mkoa wa Manyara Honest Themba amesema kila eneo la taasisi au sehemu ya kazi kuwepo na tawi la Baraza la Wafanyakazi.
Mkuu wa mkoa wa Manyara Charles Makongoro Nyerere amesema changamoto zilizopo chini ya uwezo wake atazitafutia ufumbuzi na zile zilizo nje ya uwezo wake ataziwasilisha ngazi zingine.
Amesema serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan Ina nia ya dhati ya kishughulikia changamoto zote zinazowakabili Wafanyakazi.
Toa Maoni Yako:
0 comments: