KATIBU Mkuu Wizara ya Kilimo, Andrew Massawe amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa kutuma wataalamu kutoka Tume hiyo kufika katika Skimu ya asili ya Udagaji iliyopo katika Halmashauri ya Mlimba kwa ajili ya kufanya usanifu na upembuzi yakinifu ili Serikali iweze kujenga mradi huo.

Massawe ametoa agizo hilo baada ya yeye na Katibu Mkuu Ulinzi, Dk Faraj Mnyepe kufika katika Skimu hiyo kufuatia maombi yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo hilo, Godwin Kunambi kwa Serikali yakiomba kupatiwa fedha kwa ajili ya mradi huo mkubwa wa umwagiliaji katika Skimu ya asili ya Udagaji.

Akizungumza mbele ya Makatibu Wakuu Wizara ya Kilimo na Ulinzi baada ya kutembelea mradi huo, Mbunge Kunambi amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kujali maendeleo ya wananchi wa Kata ya Udagaji kwa kuwatuma Makatibu hao kufika kujionea mradi huo ili Serikali iweze kuchukua hatua za kuanza ujenzi wake.

" Namshukuru Rais Samia baada ya mimi kuleta maombi ya kujengewa mradi huu alitoa maagizo kwa Wizara ya Kilimo na hapa nimshukuru Waziri Hussein Bashe kwa kukutuma Katibu Mkuu kufika hapa Udagaji kujionea mradi huu ambao Serikali ikiukamilisha utawaondolea umaskini wananchi wetu.

Skimu hii kwa sasa inatumika na wananchi kwa Kilimo Cha Mpunga na Mahindi kwa kutumia umwagiliaji asili, Skimu hii ina ukubwa wa Hekta 1,935 na ikikamilika itakua na uwezo wa kunufaisha zaidi ya Kaya 6,000 kwani ina mto wa kudumu unaotiririsha maji kwa mwaka mzima," Amesema Kunambi.

Amesema wao kama wananchi wa Udagaji wanaomba kupatiwa fedha za miundombinu hiyo ili kuweza kusaidia wakulima kuinua kipato na kuongeza ajira katika Halmashauri yao ya Mlimba.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Kilimo, Andrew Massawe amempongeza Mbunge Kunambi kwa kujali maslahi ya wananchi wake na kuahidi kuwa ndani ya wiki moja watalaamu kutoka Tume ya Taifa ya Umwagiliaji watafika katika eneo hilo kuanza kazi ya kufanya usanifu na upembuzi yakinifu.

" Nakupongeza sana Mbunge Kunambi kwa namna ambavyo umekua ukipigania maslahi ya wananchi wako, umeibua hoja ya ujenzi wa Skimu hii kwetu Serikali na tumefika hapa tumejionea, nikuhakikishie ndani ya wiki moja wataalamu kutoka Tume ya Umwagiliaji watafika hapa kuanza kazi ya usanifu na upembuzi yakinifu," Amesema Massawe.
Kajunason Blog

Kajunason Blog

A Tanzanian blog operating since October 2007, covering Local News, Politics, Fashion, Social Scenes, Interviews, Movies, Events, personalities and anything positive happening worldwide. Written in Swahili and English targeting both Swahili and English readers / viewers.

Toa Maoni Yako:

0 comments: